MTANDAO wa Wanawake na Katiba
umevitaka vyombo vya habari kuacha kuyumbushwa na upepo wa kisiasa
katika suala zima la kupigania mambo ya msingi kwa jamii ambayo
yanaitaji kuingizwa kwenye Katiba mpya kwenye mchakato unaoendelea hivi
sasa wa kuandika katiba mpya.
Kauli hiyo imetolewa na baadhi ya
wajumbe wanaounda mtandao huo jijini Dar es Salaam walipokuwa
wakizungumza na wahariri wa vyombo vya habari kuelezea msimamo wa
wajumbe hao kwenye mchakato wa uandikaji katiba mpya.
Mwakilishi kutoka Asasi ya
Wanawake ya Ulingo, Dk. Avemaria Semakafu aliviomba vyombo vya habari
kuwaunga mkono wanamtandao hao ambao pamoja na mambo mengine wamejipanga
kupigania kero za wananchi kuhakikisha zinapata majibu katika mchakato
wa uundaji katiba mpya hivyo kuwataka wanahabari kuwaunga mkono.
Alisema vyombo vya habari
visikubali kupelekeshwa na wanasiasa kwa kupaza sauti kwenye maslahi ya
wanasiasa zaidi na kushindwa kujadili masuala ya msingi ya jamii, ambayo
endapo yatapata majibu katika mchakato wa uundaji katiba mpya
wananufaika ni wananchi wote tofauti na masuala ya utawala (madaraka).
“Waandishi wa habari msikubali
kuchezeshwa ngoma za wanasiasa, ambao mara zote wanapigania maslahi yao
kiutawala…tupiganie maslahi ya jamii, jamii inaitaji kuona huduma bora
za afya, elimu na mgawanyo sawa wa rasilimali,” alisema Dk. Semakafu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi
Mtendaji wa TAMWA, Valerie Msoka taasisi moja wapo inayounda Mtandao wa
Wanawake na Katiba akiwasilisha mada kwa wahariri wa vyombo mbalimbali
vya habari alisema vyombo vya habari vina nguvu za kipekee katika kuleta
mabadiliko kwenye jamii na mamlaka hivyo kuwaomba watumie fursa hiyo
ipasavyo katika kupigania maslahi ya umma.
“…Hivyo vyombo vya habari, kama
msingi wa kupatikana kwa taarifa yoyote, na kuongoza katika ushawishi
vina sehemu muhimu sana katika kuongoza kuleta mabadiliko yawe ya sera,
tabia au utamaduni,” alisema Bi. Msoka ambaye pia ni Mjumbe wa Bunge la
Katiba.
Hata hivyo alivitaka vyombo vya
habari kuwaunga mkono wanawake kwani licha ya kuwa na mchango mkubwa
katika jamii wamekuwa wakikabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo za
kusahaulika kwenye fursa anuai zilizopo. “…Wanawake ni asilimia 80 ya
nguvu kazi vijijini na ni asilimia 60 ya wazalishaji wakuu wa
chakula…lakini tunachangamoto nyingi,” alisema Bi. Msoka.
Mtandao wa Wanawake na Katiba ni
muunganiko wa asasi za kijamii na kitaaluma zipatazo hamsini
zilizoungana kudai katiba inayozingatia masuala ya kijinsia na
inayotokana na mchakato ulioshirikisha sauti za makundi yote.
*Imeandaliwa na www.thehabari.com
إرسال تعليق