KESI YA DK MAHANGA DHIDI YA MSEMAKWELI YAFUTWA

Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imeifuta kesi ya madai ya kashfa iliyokuwa imefunguliwa na Naibu Waziri wa Kazi na Ajira,  Dk Makongoro Mahanga dhidi ya Mwanaharakati, Kainerugaba Msemakweli na wenzake.
Jaji Salvatory Bongole alitoa uamuzi huo jana wakati kesi hiyo ilipotajwa, kwa sababu Dk Mahanga na Wakili wake hawakufika mahakamani hapo.
Mahanga alifungua kesi hiyo namba 145/2009 akidai wadaiwa walichapisha habari iliyomdhalilisha kwa kueleza amegushi vyeti vya elimu ya juu magazetini.
Akitoa uamuzi huo, Jaji Bongole alisema amefuta kesi hiyo kwa gharama kwa kuwa Dk Mahanga na Wakili wake Kennedy Fungamtama hawafiki mahakamani bila kutoa taarifa na hakuna ushahidi wa wito wa kuitwa mahakamani umekua ukiwafikia kwa wakati.
Mbali na Msemakweli wadaiwa wengine ni mwandishi wa gazeti la Nipashe, Muhibu Saidi, Mhariri Mtendaji wa Gazeti hilo na Kampuni ya The Guardian Limited waliokuwa wanatetewa na Wakili wa kujitegemea.
Kwa mujibu wa hati ya Madai, Dk Makongoro alikuwa akiomba wadaiwa wamlipe  Sh bilioni tatu kama fidia ya madhara aliyoyapata kutokana na habari ya uongo iliyochapishwa na wadaiwa.
Habari hiyo ilichapishwa katika Gazeti la Nipashe la Oktoba 19 Mwaka 2009 iliyokuwa na kichwa cha habari kisemacho: " Vyeti Vya Elimu: Mawaziri Sita wanasa"

Post a Comment

أحدث أقدم