Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa iliyowekwa hivi karibuni katika Tovuti ya Ofisi ya Takwimu ya Taifa, imefafanua kwa undani historia ya mafanikio ya sekta hiyo muhimu kwa maisha ya kiuchumi ya Watanzania na uwezekano huo katika siku za hivi karibuni.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kuna baadhi ya miamba inayozalisha gesi asilia, ipo katika mipaka ya nchi mbili na imefafanuliwa kuwa: “Jiolojia ya miamba haina mipaka kati ya leseni moja na leseni nyingine (ndani ya nchi), pia nchi moja na nchi nyingine.”
Nchi zilizotajwa kuwa na miamba hiyo katika mpaka wake na Tanzania ni Msumbiji, Malawi, Kenya na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
“Hivyo ili kukabiliana na changamoto hii, mazungumzo ya uzalishaji wa pamoja yatafanyika katika maeneo yenye muingiliano wa rasilimali za mafuta au gesi asilia,” imeeleza taarifa hiyo.
Taarifa hiyo pia imeweka katika takwimu mafanikio ya gesi, ambayo ndiyo sekta muhimu ya matumaini katika uchumi wa Tanzania na wananchi.
“Uwepo wa nishati ya gesi nchini na shughuli zinazohusu utafutaji, uchimbaji na usambazaji wa gesi asilia zimekuwa na manufaa makubwa kwa Taifa.
“Manufaa hayo yanajumuisha kupunguza gharama za matumizi ya mafuta, kupunguza uchafuzi wa mazingira, kutoa ajira na kuongeza mapato kwa Serikali na halmashauri za wilaya,” imeeleza ripoti hiyo.
Sehemu kubwa ya mafanikio hayo, inatokana na matumizi ya gesi kidogo tu kutoka katika vyanzo vya gesi vilivyoanza uzalishaji ambavyo vipo katika nchi kavu, ambavyo ni mbali na ugunduzi mkubwa uliofanyika baharini uliosababisha Tanzania kuwa miongozi mwa nchi zinazotarajiwa kuwa za uchumi wa gesi
Taarifa hiyo imeeleza kuwa mpaka sasa, gesi asilia iliyogundulika baharini ni kiasi cha futi za ujazo trilioni 38.5 na nchi kavu ni futi za ujazo trilioni 8.
Hata hivyo hivi karibuni katika Bunge lililopita, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, alisema Tanzania kumegundulika gesi futi za ujazo trilioni 50.5, sawa na mapipa bilioni 9.6.
Aliwataka Watanzania wasisikilize hoja za watu wanaopotosha baada ya kupata mafunzo ya wiki moja nje ya nchi, kwa kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha katika mgawo wa mapato ya gesi, Serikali itakuwa ikipata kati ya asilimia 62.95 mpaka asilimia 82.5.
Aidha taarifa hiyo imewataka Watanzania kuvuta subira kwamba mafanikio zaidi yanakuja, kwa kuwa miundombinu ya miradi ya gesi huchukua kipindi kirefu kati ya miaka mitano mpaka saba tangu kugunduliwa mpaka kutumika kwa nishati hiyo.
Katika sekta ya umeme, taarifa hiyo iliyoainisha mafanikio hayo kutokana na matumizi ya gesi ya nchi kavu zaidi, imefafanua kuwa uchumi wa Tanzania, unakadiriwa kupoteza zaidi ya Sh trilioni moja na nusu kwa mwaka, kwa kutumia mafuta badala ya gesi asilia kwa mitambo ya kufua umeme.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, uzalishaji wa nishati kwa kutumia gesi ni wa gharama ya chini ikilinganishwa na uzalishaji wa nishati hiyo kwa kutumia mafuta.
Kwa mfano uzalishaji wa kipimo kimoja cha nishati cha mmBtu kwa kutumia mafuta, kwa mujibu wa taarifa hiyo ni dola za Marekani 32, wakati uzalishaji wa kipimo hicho hicho cha nishati ya umeme kwa kutumia gesi, gharama yake ni dola za Marekani 1.6 tu.
Kwa kutumia bomba lililopo la gesi, linalosafirisha rasilimali hiyo mpaka Dar es Salaam kutoka Songo Songo na ile inayotumika Mtwara, nchi imeendelea kuokoa fedha za kigeni katika kuzalisha umeme na matumizi ya viwandani.
Taarifa hiyo imeonesha kuwa kuanzia Julai 2004 hadi Desemba 2013, futi za ujazo bilioni 196.6 za gesi asilia zenye thamani ya dola za Kimarekani milioni 322.4 zilitumika kuzalisha nishati iliyotumika katika uzalishaji umeme.
Imeelezwa kuwa nishati hiyo kama ingezalishwa kwa kutumia mafuta, ingegharimu kiasi cha dola za Kimarekani bilioni 6.4.
“Kwa sababu hiyo, kwa matumizi ya gesi asilia katika uzalishaji umeme, Serikali imeokoa kiasi cha dola za Marekani bilioni 6.1 kutoka gesi ilipoanza kuzalishwa mpaka mwishoni mwa mwaka jana,” ilieleza taarifa hiyo.
Kwa upande wa matumizi ya viwandani, kuanzia Julai 2004 mpaka Desemba 2013, gesi asilia yenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 238.8 ilitumika kama nishati mbadala kuendeshea mitambo ya viwanda hivyo.
Taarifa hiyo imebainisha kuwa kuzalisha nishati hiyo kwa kutumia mafuta kwa kipindi hicho chote, ingegharimu Dola za Kimarekani milioni 713.
“Hivyo, kwa matumizi ya gesi asilia viwandani, kiasi cha Dola za Kimarekani milioni 474.2 kimeokolewa,” ilieleza taarifa hiyo.
Vile vile, matumizi ya gesi badala ya mafuta kwenye taasisi, majumbani na katika magari yameokoa fedha za kigeni kwa kiasi kikubwa.
“Kuanzia Desemba 2009 mpaka Desemba 2013, gesi asilia yenye thamani ya Dola za Kimarekani 819,907 ilitumika kuzalisha nishati kiasi cha mmBtu 37,705 ambapo kama nishati ya mafuta ingetumika ingegharimu kiasi cha Dola za Kimarekani 981,718.
“Hivyo, katika kipindi husika, Serikali iliokoa kiasi cha Dola za Kimarekani 161,811 kwa matumizi ya gesi asilia katika taasisi, majumbani na katika magari,” imeeleza taarifa hiyo.
Bomba jipya la gesi kutoka Mtwara likifika Dar es Salaam, Serikali inatarajia bei ya umeme kupungua kutokana na matarajio ya kupungua kwa bei ya umeme kutoka kampuni zinazofua umeme na kuboresha maisha ya Watanzania kwa kuuziwa umeme nafuu na kuvutia viwanda kutokana nishati nafuu.
Kwa sasa kampuni zinazomiliki mashine za kufua umeme, zinauza uniti moja ya umeme Shirika la Umeme (Tanesco), kwa senti za Marekani 33 mpaka 60.
Tanzania kwa sasa inatumia megawati 1,850 za umeme ambazo kwa mujibu wa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda asilimia 80 zinazalishwa kwa mafuta ya dizeli na mafuta mazito na asilimia nyingine ndizo zinazotokana na vyanzo vingine vya maji na gesi ya Songosongo.
Serikali inatarajia mara bomba la gesi kutoka Mtwara likimalizika kujengwa na uzalishaji kuanza Dar es Salaam, Tanesco itanunua umeme huo kwa senti 8 na kufanya nishati hiyo bei yake kushuka.
“Hii bei ya umeme iliyopo kwa sasa ni kwa muda tu na itashuka sana bomba la gesi likikamilika kwa sababu hata mitambo ya kufua umeme inayotumia mafuta nayo itatumia gesi na mitambo mipya ya gesi italetwa, nataka Watanzania wakubali hivyo,” aliwahi kusema Profesa Muhongo.
Manufaa mengine yaliyotokana na matumizi ya gesi kidogo tu iliyotumika mpaka mwaka jana, ni pamoja na kupunguza kwa kiasi kikubwa uchafuzi wa hali ya hewa unaotokana na matumizi ya mafuta katika uzalishaji umeme, viwandani na katika taasisi.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kiasi cha tani milioni 13.4 cha hewa ukaa (Co 2) huzalishwa katika uzalishaji wa umeme kwa mitambo itumiayo mafuta aina ya Jet 1, wakati matumizi ya gesi asilia huzalisha tani milioni 10.1 za hewa ukaa.
“Hivyo, matumizi ya gesi asilia yamepunguza uchafuzi wa hewa kwa takriban tani milioni 3.3 za hewa ukaa. Kwa upande wa viwandani, matumizi ya mafuta mazito (HFO) huzalisha hewa ukaa kiasi cha tani milioni 3.5 wakati matumizi ya gesi katika viwanda huzalisha tani milioni 2.1 za hewa ukaa, hivyo punguzo la hewa chafu ni tani milioni 1.4,” imeeleza.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, hata matumizi ya gesi aina ya LPG yanayoagizwa kutoka nje ya nchi kwa ajili ya taasisi, hewa ukaa kiasi cha tani 2,215.43 huzalishwa ikilinganishwa na matumizi ya gesi asilia ambapo kiasi cha tani 1,860.35 za hewa ukaa huzalishwa ikiwa ni punguzo la hewa chafu kwa tani 355.08.
“Hivyo kwa wastani matumizi ya gesi asilia hupunguza hewa chafu kwa zaidi ya asilimia 25 ikilinganishwa na matumizi ya mafuta,” ilieleza taarifa hiyo.
إرسال تعليق