MFUMUKO WA BEI WAPUNGUA HADI ASILIMIA 6.4

Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imesema mfumuko wa bei wa taifa kwa mwezi Juni umepungua hadi asilimia 6.4 kutoka asilimia 6.5 ilivyokuwa  mwezi Mei mwaka huu.
Mkurugenzi wa Takwimu za Jamii na Sensa ya Watu na Makazi wa NBS, Ephraimu Kwesigabo, alisema jana kuwa  hali hiyo inamaanisha kuwa kasi ya upandaji wa bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia Juni imepungua ikilinganishwa  na kasi iliyokuwepo mwezi Mei.
Hata hivyo, Kwesigabo alisema fahirisi za bei zimeongezeka hadi 148.98 kwa mwezi wa Juni kutoka 140.00 Juni 2013.  Alisema mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi umepungua hadi asilimia 8.1 Juni kutoka asilimia 8.7 ilivyokuwa Mei mwaka huu.
Mkurugenzi huyo alisema badiliko la Fahirisi za bei za bidhaa za vyakula nyumbani na migahawani, imepungua hdi asilimia 8.7 kutoka asilimia 9.3 ilivyokuwa Mei wakati badiliko la fahirisi za bei kwa bidhaa zisizo za vyakula, limeongezeka hadi asilimai 4.8 Juni kutoka asilimia 4.1 Mei mwaka huu.
Akizungumzia mfumuko wa bei kwa kipimo cha mwezi, Kwesigabo alisema umepungua kwa asilimia 0.6, ikilinganishwa na kupuungua kjwa asilimai 0.4 kama ilivyokuwa Mei.
Fahirisi za bei katika kipindi hicho, pia zimepungua hadi 148.98 mwezi Juni kutoka 149.89 Mei mwaka huu. Kupungua kwa fahirisi hizo, kumechangiwa hasa na kupungua kwa bei za bidhaa za vyakula.
Alitaja baadhi ya bidhaa za vyakula, zilizochangia kupungua kwa fahirisi ni pamoja na mchele asilimia 3.0, mahindi asilimia 12.3, unga wa mahindi asilimia 3.5, muhogo kwa asilimia 8.9.
Bidhaa nyingine ni viazi vitamu asilimia 9.1, dagaa kwa asilimia 4.1, matunda jamii ya machungwa asilimia 14.4, mbogamboga asilimia 1.2 na vitunguumaji kwa asilimia 2.5.
Kuhusu thamani ya shilingi ya Tanzania katika kununua bidhaa na huduma kutoka mwezi Septemba 2010,  alisema imeongezeka hadi Sh 67 na senti mwezi Juni kutoka Sh 66 na senti 72 Mei, mwaka huu.
Mkurugenzi huyo alisema fahirisi za nishati na mafuta na fahirisi za vyakula na vinywaji baridi, zimekuwa na mwenendo wa juu kwa kipindi chote, zikilinganishwa na fahirisi nyingine.
"Kundi la nishati na mafuta limeonesha pia kuwa na mwenendo wa fahirisi usio imara ikilinganishwa na makundi mengine kwa kipindi husika," alisema Kwesigabo.
Aliongeza kuwa fahirisi za bidhaa zisizo za chakula na fahirisi za bidhaa zisizo jumuisha chakula pamoja na nishati, zimeonesha mwenendo wa bei ulio imara.

Post a Comment

أحدث أقدم