Hayo yalisemwa na Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Seif Sharif Hamad wakati alipofanya ziara kwenye masoko mbalimbali.
Alisema kama wafanyabiashara watapunguza bei ya vyakula mbali mbali katika kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadhani, basi watajipatia thawabu kutoka kwa Mungu.
Hata hivyo alieleza kufurahishwa na kuwepo kwa vyakula vingi. ''Nimefurahishwa na wingi wa vyakula katika kipindi hichi cha mwezi mtukufu wa Ramadhani na hivyo kutoa nafasi kwa wananchi kufunga vizuri,"alisema.
Miongoni mwa masoko aliyotembelea ni pamoja na la Mwanakwerekwe. Alitembelea pia soko la samaki lililopo Malindi na kuwataka watumiaji wake kuimarisha usafi kwa ajili ya afya za walaji.
Alisema bado lipo tatizo la upungufu wa samaki zaidi katika kipindi hiki cha mabadiliko ya tabia ya nchi yanayotokana na upepo mkali unaovuma katika majira ya jioni na kuwafanya wavuvi kuacha kwenda baharini.
Baadhi ya wakulima waliozungumza katika soko kuu la Mwanakwerekwe walilalamika tatizo la wizi wa mazao katika mashamba ya wakulima zaidi wilaya ya kati Unguja.
Juma Haji mkulima katika kijiji cha Kitumba wilaya ya kati Unguja alisema wanakabiliwa na wizi wa mazao unafanyika usiku ikiwemo kuangusha nazi na kuwafanya wakulima wakati mwengine kuvuna mazao yakiwa machanga.
Post a Comment