Watu
wawili wanaotuhumiwa kuhusika na tukio la kushambulia gari la magereza
kwa risasi, wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi
Kinondoni wakikabiliwa na mashitaka matatu.
Watuhumiwa hao, Peter
Mushi (36) dereva na Godlisten Mongi (40) ambaye hati ya mashitaka
imemtambulisha kwamba ni mhandisi, walipandishwa kizimbani jana kwa
mashitaka ya kula njama, unyang’anyi wa kutumia silaha na shambulio la
kudhuru mwili.
Wakili wa Serikali, Matarasa Alungo alidai mbele ya
Hakimu Anipha Mwingira kwamba Julai 2 mwaka huu, maeneo ya Mikocheni
karibu na Hospitali ya Regency, Kinondoni, washitakiwa walikula njama
kufanya uhalifu.
Alungo alidai katika mashitaka ya pili Mushi na
Mongi waliwavamia askari wa magereza WP 481 CPL Dotto na Dorin Damas na
kuwapiga kwa kutumia silaha ya moto.
Katika mashitaka ya tatu, alidai
watuhumiwa hao walimshambulia kwa kumpiga Dorin katika uso wake na
kumsababishia maumivu mwilini.
Washitakiwa walikana mashitaka hayo na
upelelezi wa shauri hilo haujakamilika. Walirudishwa rumande baada ya
kushindwa masharti ya dhamana na kesi itatajwa tena Agosti 8 mwaka huu.
Wakati
huohuo, watuhumiwa Mushi na Mongi wamepandishwa tena kizimbani katika
mahakama hiyo, wakikabiliwa na mashitaka ya mauaji.
Mshitakiwa wa
tatu katika kesi hiyo, raia wa Burundi, Maulid Nkurunziza (23)
hakusomewa shitaka mahakamani hapo baada ya Wakili Musini Mussa kueleza
kuwa yupo gerezani na angefuatwa huko kusomewa shitaka lake.
Mussa
alidai mbele ya Hakimu Joyce Mushi kwamba, Mei 23 mwaka huu, maeneo ya
Kunduchi Silver Wilaya ya Kinondoni, washitakiwa walimuua Edwin
Humphrey, dereva wa pikipiki.
Washitakiwa wawili hawakutakiwa kujibu
chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka kusikiliza kesi ya mauaji.
Washitakiwa walirudishwa rumande hadi Agosti 8 mwaka huu.
إرسال تعليق