Kamati ya Usalama na Maadili ya CCM inatarajiwa kukutana mwezi ujao kupitia mwenendo wa utekelezaji wa adhabu kwa wanachama hao kabla ya kutoa mapendekezo kwa Kamati Kuu kuchukua hatua kulingana na uvunjaji masharti ya adhabu.
Makada hao sita ambao Februari mwaka huu walipewa adhabu ya onyo na kuwa chini ya uangalizi wa mwaka mmoja wa kujirekebisha mwenendo wao, baadhi yao wanadaiwa kukiuka masharti ya adhabu hiyo kwa kuendelea kutangaza nia, jambo ambalo linaashiria wanaweza kuongezewa adhabu zaidi.
Akizungumzia ajenda zilizojadiliwa na Kamati Kuu iliyokutana juzi jijini Dar es Salaam, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye alisema Kamati ya Usalama na Maadili ya CCM itakapokutana itapitia mwenendo wa utekelezaji wa adhabu kwa wanachama hao waliopewa adhabu.
“Kamati ya Usalama na Maadili itapitia mwenendo wa utekelezaji wa adhabu, na kama itabainika kuwa hawatekelezi ipasavyo masharti ya adhabu, itapendekeza kwa Kamati Kuu kuongezwa kwa adhabu kulingana na ukubwa wa uvunjaji masharti ya adhabu,” alisema Nape.
Nape alisema, “Kamati Kuu ilipokea taarifa za harakati za baadhi ya wanachama wa CCM walioonesha nia ya kuomba ridhaa ya chama kugombea urais, baada ya kutafakari kwa kina kamati inawakumbusha wote kuwa ili wasipoteze sifa za kugombea ni muhimu wakazingatia Katiba, Kanuni na taratibu za chama zinazosimamia masuala ya uchaguzi.”
Alisisitiza, “Wanachama wanatakiwa kukumbuka kuwa chama ni pamoja na Katiba, kanuni na taratibu zake. Kutoziheshimu na kuzifuata ni kukivuruga, jambo ambalo halivumiliki.”
Kwa mujibu wa kanuni za CCM, wanachama watakaobainika kukiuka katiba, kanuni na taratibu za chama zinazosimamia masuala ya uchaguzi, wanaweza kukutwa na adhabu ya kufungiwa kwa muda au kukosa sifa na kuondolewa kwenye kinyang’anyiro.
Hivi karibuni, baadhi ya wanachama walio katika ‘kifungo’, wamekaririwa wakitangaza nia ya kuwania urais.
Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba ni miongoni, ambaye wakati akihojiwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), alisema ana uhakika wa kugombea urais kwa asilimia 90.
Wengine ambao wanadaiwa kuendelea kutangaza nia ni Waziri wa Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe na Waziri Mkuu Mstaafu, Fredrick Sumaye.
Licha ya Makamba, Membe na Sumaye, makada wengine walio chini ya uchunguzi wakiangaliwa mienendo yao, ni Edward Lowassa, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu, Stephen Wassira na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.
Wana CCM hao walipewa adhabu hiyo baada ya kuhojiwa na kukutwa na makosa. Walihojiwa na Sekretarieti ya CCM mjini Dodoma, kabla ya Tume ya Udhibiti na Nidhamu kuwajadili na hatimaye Kamati Kuu ya CCM kutoa adhabu kwao.
Walipohojiwa, wote walithibitika kuanza kampeni za kutafuta kuteuliwa kugombea urais kabla ya wakati, jambo ambalo ni kinyume na Kanuni za Uongozi na Maadili za CCM toleo la Februari 2010, Ibara 6(7)(i)
Katika hatua nyingine, akizungumzia ajenda nyingine zilizojadiliwa na Kamati Kuu juzi, Nape alisema nia ya chama ni kusimamia na kuhakikisha kinakuwa na umoja ambao ni muhimu hasa katika kuelekea kukamilisha kazi ya utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi wa 2010/20 na uchaguzi wa mwaka 2015.
إرسال تعليق