
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili shuleni hapo hivi karibuni umebaini kuwa, unyama huo umekuwa ukifanywa na vijana ambao huwarubuni watoto hao kwa kuwapatia fedha kidogo kati ya Sh. 2,000 hadi 7,000 kisha kuwaingilia kinyume cha maumbile.
NIPASHE Jumapili imebaini kuwa, vitendo hivyo vimekuwa vikifanywa na vijana hao ambapo mara baada ya kuwarubuni kwa zawadi ndogo, huwapeleka kwenye chumba kisha kuwalawiti na kuwatisha wasiseme kwa mtu yeyote.
NIPASHE ilifika shuleni hapo na kujionea mazingira hatarishi kwa wanafunzi wa shule hiyo na nyingine iliyopo jirani na Shule ya Msingi Manzese ambapo nje ya milango ya kutokea kumezungukwa na
nyumba za kulala wageni.
Katika mahojiano na gazeti hili, Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Biamina Swai, alithibitisha kutokea kwa matukio hayo manne ndani ya mwaka huu.
Aidha, alisema kati ya matukio hayo, moja tu ndiyo mtuhumiwa wake alikamatwa Jumatatu ya wiki hii baada ya kuwekewa mtego.
Alisema matukio mengine wahusika walitoroka baada ya wazazi wa watoto kuvujisha siri mtaani kabla ya kukamatwa kwao huku la mwanafunzi wa darasa la tatu (jina linahifadhiwa) mtuhumiwa wake akishikiliwa katika Kituo cha Polisi cha Urafiki.
Akielezea jinsi walivyombaini mtoto huyo, Swai alisema wiki iliyopita mwalimu wa darasa analosoma mwanafunzi huyo, alimkuta akiwa na Sh. 7,000.
“Alipobanwa na mwalimu pamoja na wenzake darasani ili aeleze amezipata wapi, ndipo mwanafunzi huyu alipofunguka na kueleza hupewa na kijana mmoja mtaani ambaye mara baada ya kumfanyia mchezo huo humpa hela,” alisema.
Alisema kijana huyo ambaye ametajwa kwa jina moja la Enock amekuwa akimpeleka kwenye chumba chake kilichopo maeneo hayo kisha kumfanyia kitendo hicho kinyume cha maumbile.
Aliongeza kuwa, mtoto huyo alisema mbali ya hela aliyokutwa nayo, aliwahi kupewa Sh. 5,000 na Sh.2,000 mara baada ya kufanyiwa hivyo.
“Tulipopata maelezo ya mtoto huyu tuliendelea kuwahoji wengine, ndipo mwanafunzi mwingine wa kike mwenye umri wa miaka nane (jina linahifadhiwa) akatueleza amekuwa akichukuliwa na kijana mwingine ambaye anauza mapazia katika soko la Argentina na kumfanyia mchezo huo,” alisema.
Swai alisema baada ya maelezo hayo waliwasiliana na wazazi wa watoto hao ambapo, mzazi mmoja ndiye aliyeweza kufanikisha kukamatwa kwa mtuhumiwa.
Alisema wazazi wengine mara baada ya kupewa taarifa hizo shuleni hapo, walipofika mtaani na kuvujisha siri na kusababisha wahusika kukimbia.
“Tunapobaini haya huwa tunapenda kuwashirikisha wazazi wao ili kwa pamoja tufanikishe kukamata watuhumiwa, ila tunapowapa taarifa za watoto wao huwa wanachanganyikiwa na kujikuta wakivujisha siri,” alisema.
Alisema wanafunzi ambao hukumbwa na tatizo hilo ni kuanzia darasa la kwanza hadi la nne ambao kiumri ni wadogo na rahisi kurubuniwa na genge hilo la vijana.
Alisema kutokana na kushamiri kwa matendo hayo, mwezi Julai, mwaka huu walitoa mafunzo ya uelimishaji rika ambayo yalihusisha walimu wa afya na wanafunzi.
Akizungumzia kuhusu wazazi, alisema asilimia kubwa ya wazazi hawana nafasi ya kukaa na kuzungumza na watoto wao pindi wawapo majumbani ndiyo maana wamekuwa hawabaini.
“Mzazi akiwa karibu na mtoto wake ni rahisi kubaini tofauti zilizopo kwa mwanae, lakini wazazi wengi wapo bize wanatafuta fedha kuliko kuangalia maendeleo na mienendo ya watoto wao, hawa watoto wazazi wao wangekuwa karibu nao wangebaini haya mapema,” alisema.
Aliwataka wanafunzi kuacha tamaa ya zawadi na fedha kwa kuwa wakati wao bado. Mzazi wa mwanafunzi (jina linahifadhiwa) ambaye mtuhumiwa wake amekamatwa, alisema siku ambayo mtoto wake alipokutwa na Sh. 7,000 alipigiwa simu na mwalimu wake wa darasa.
“Mwalimu alinitaka niende shuleni hapo nilipofika aliniambia kuwa kuna kijana anampatia fedha mwanangu na kumfanyisha mchezo huo, nilimbana anionyeshe aliniahidi kufanya hivyo, aliniambia wanapofika chumbani mwanaume huyo hukaa kwenye kochi na kumpakata kisha kumfanyia mchezo huo," alisema.
Alisema Jumatatu ya wiki hii aliambatana na mtoto wake hadi eneo la tukio ambapo kabla ya kukamatwa kwake, alimwonyesha kwa mbali mhusika.
“Wakati tunakaribia eneo alikokuwa amesimama mtuhumiwa ambaye wakati huo alikuwa na wenzake watatu, mwanangu aliniambia kwa kilugha 'kijana mwenyewe ni yule pale', basi nilimwambia atangulie mbele amfuate,” alisema na kuongeza: "Kabla hajamkaribia yule kijana alimfuata, wakati huo na mimi nilikuwa nimefika eneo la tukio na kujifanya nachezea simu, kijana alimuuliza mwanangu leo nikupe shilingi ngapi, mwanangu akajibu Sh. 200, wakati akimpa nilisogea karibu na kumuuliza kijana kwa nini anampa hela mtoto wangu na kwa nini anamfanyia vitendo viovu,” alisema baada ya kumhoji aliomba msaada kwa watu na kupiga simu kwenye shule ambayo mtoto wake anasoma ili wamsaidie.
Gazeti hili lilifanikiwa kufika kwenye kituo cha Polisi cha Urafiki, ambapo mkuu wa kituo hicho ambaye alisema siyo msemaji wa polisi, alithibitisha kuwapo kwa tukio hilo ambalo uchunguzi wake unaendelea.
NIPASHE pia ilifanikiwa kwenda Shule ya Msingi ya Manzese ambayo mmoja wa walimu waliokutwa hapo alisema kuwa katika shule hiyo hakuna matukio hayo.
IPP NIPASHE Jumapili: Ulawiti watishia shule jijini Dar
إرسال تعليق