
Ndugu zangu,
LEO ni Septemba 19, ni Siku ya Kuzaliwa Mtandao wa Mjengwablog.
Kwa mwanadamu, hakupaswi kuwapo na ukomo wa kujitahidi kufanya yalo mema kwa jamii yako.
Na
katika kujitahidi kuyafanya yalo mema, basi, mwanadamu uwe tayari
kukumbana na changamoto nyingi. Na kama ilivyo kwa maji ya mto,
yanapokutana na mwamba, basi, kasi yake huongezeka maradufu.
Leo
blogu yako hii ya Mjengwablog imetimiza miaka minane. Miaka minane si
haba. Kwa mtoto, aweza kuwa darasa la Pili. Na kwetu wa Mjengwablog ni
miaka minane ya kujifunza, kukosea, kujifunza kutokana na makosa, na
kisha kusonga mbele.
Kwa
niaba ya timu nzima ya Mjengwablog nachukua fursa hii kuwashukuru,
kwanza kabisa, mke wangu mpenzi, Mia, ambaye, bila yeye, kazi hii yangu
ya kuitumikia jamii ingelikuwa ngumu sana. Pili, niwashukuru kwa dhati
wanangu wanne, Olle, John, Manfred na Gustav. Wanawangu hawa wamekuwa na
mchango mkubwa pia, ikiwamo kufanya utani na mimi baba yao, ilimradi
niwe na wakati wa kucheka, hata pale nilipoona kazi ni ngumu na kukutana
na vikwazo.
Na
kwa dhati kabisa, naishukuru timu nzima ya Mjengwablog. Nawashukuru kwa
upekee kabisa Wanafamilia wote wa Mjengwablog, ukiwamo wewe unayesoma
maandiko haya sasa, maana, bila nyinyi, kusingekuwa na maana ya kuifanya
kazi hii. Mmekuwa nasi katika hali zote. Hivyo basi, kutuunga mkono.
Naam,
ni miaka minane ya kuwa mtandaoni karibu katika kila siku inayotujia na
kupita. Ni miaka minane ya mapambano magumu ya kuitumikia jamii na
kuhakikisha kuwa tunabaki hai.
Maana,
unapoamua kuitumikia jamii bila kuegemea upande, basi, ina maana pia ya
kujiweka katika mazingira ya hatari sana. Yumkini kuna maua mengi ya
upendo yanaweza kurushwa kwako, lakini, kuna mishale michache ya sumu
ambayo pia itarushwa kwako. Kwamba kuna maadui pia.
Na
ukimwona nyani ametimiza miaka minane , basi, ujue kuna mishale kadhaa
ameikwepa. Lakini, na anavyozidi kuendelea kuishi, yumkini kuna mishale
mingine inaandaliwa. Na nyani hatakiwi kuishi kwa kuogopa mishale ya
wanadamu. Vinginevyo, ajitundike mtini, afe.
Lililo
jema na kutia faraja ni kutambua, kuwa kuna walio wengi wenye kufaidika
na kazi hii ya kijamii ambayo Mjengwablog inaifanya. Ni hawa ndio wenye
kututia nguvu ya kuendelea kuifanya kazi hii pamoja na changamoto zake
nyingi.
Ndugu zangu,
Ilikuwa
ni Jumanne, Septemba 19, 2006. Ni siku hiyo ndipo kwa mara ya kwanza
niliingiza picha ya kwanza kwenye mjengwablog na kuashiria uzinduzi wa
blogu. Ni picha hiyo inayoonekana hapo juu. Niliipiga eneo la Kinondoni
Shamba. Tangu siku ya kwanza, niliweka wazi kwenye fikra zangu, kuwa
Mjengwablog iwe jukwaa litakalomtanguliza mtu wa kawaida. Iwe sauti ya
wale ambao sauti zao hazisikiki.
Na
Mjengwablog ikawa chachu ya kuanzishwa kwa gazeti la michezo na burudani
la ’ Gozi Spoti’, ikawa chachu pia ya kuanzishwa gazeti la ’ Kwanza
Jamii’.
Na
kuna miongoni mwetu wenye kufikiri, kuwa mwenye kumiliki gazeti ni
lazima awe Mhindi au Mtanzania ’ mweusi’ Mfanyabiashara tajiri.
Nakumbuka kuna hata ambao hawakuwa tayari kuchangia kiuandishi kwenye ’
Gozi Spoti’ na ’ Kwanza Jamii’ kwa vile linamilikiwa na ’ Mswahili
mwenzao!’Na hata kupata matangazo kukawa na ugumu mkubwa. Gozi Spoti
lilisimama kuchapwa baada ya mwaka mmoja mitaani. Kwanza Jamii, nalo
likasimama kuchapwa. Likarudi tena baada ya kuingia ubia na Shirika la
Daraja. Baada ya miaka miwili na baada ya aliyepelekea kuingia ubia
kuondoka nchini na kurudi kwao Uingereza, basi, Kwanza Jamii nalo ’
likaandaliwa’ mazingira ya kuondoka mitaani.
Hata
hivyo, Kwanza Jamii, gazeti dogo, ambalo naamini ni muhimu kwa jamii,
limerudi tena kwa kutolewa bure kanda ya Nyanda za Juu Kusini na kwa
kupitia mtandaoni. Mipango iko mbioni kuliimarisha zaidi katika siku
zijazo.
Ndugu zangu,
Changamoto
zipo ili tukabiliane nazo, na si kukata tamaa. Mjengwablog inatimiza
miaka minane leo kwa vile tulishaamua, kuwa tutapambana hadi risasi ya
mwisho. Hivyo pia, tutapambana hadi pumzi ya mwisho.
Maana,
tunaamini kuwa kazi tuifanyayo ni yenye manufaa kwa jamii pana. Na tuna
haki ya kuifanya. Tunavumilia sauti zenye kutushutumu na kutukosoa.
Kuna tunayojifunza kutoka kwa wakosoaji wetu. Tunawashukuru sana na
tunawaomba waendelee kutukosoa kila wanapoziona kasoro.
Chini
hapa ni maoni ya kwanza kabisa kutumwa na mtembeleaji. Na anachoandika
mtembeleaji huyu kutoka India kinaakisi dhamira niliyokuwa nayo.
Bwana
huyu anasema; { fakir005 } at: Tue Sep 19, 06:32:00 PM EAT said… This
looks like an African blog. Once the TV showed an African milk his cow.
The cow had so stretched tits. I’ve never seen so much stretching. The
african as really stretching further to twice the original length to get
any drop of milk he could get. It was obvious the cow was dry because
it was too long after the birth of her calf and needed to be inseminated
again.The cow just stood there while the African worked the Tits. The
picture does not show anycows. But the man in the picture and the house
remind me of the TV scene in the gone years.”
Maggid,
Mwenyekiti Mtendaji.
Mjengwablog.com
إرسال تعليق