Mbunge wa Jimbo la Korongwe Mjini, Yusuph Nassir
Zomea hiyo ilifuatia baada ya Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi
(CCM), Abdulrahman Kinana, kuwataka wananchi waulize maswali kwenye
mkutano wa hadhara ili viongozi wake wayajibu.
Akijibu baadhi ya maswali aliyoulizwa na wananchi hao, mbunge huyo
aliambulia miguno na maneno ya kebehi. "Hajui huyo..., hatembelei
wananchi wake."
Hali hiyo ilimlazimu Kinana, kumuamuru Diwani wa kata hiyo, Robart Bago, kuanza kujibu baadhi ya kero zilizotolewa.
Hata hivyo, diwani huyo alijikuta katika wakati mgumu baada ya
kushindwa kujibu maswali yaliyoulizwa na kuanza kuelezea historia
mbalimbali hali iliyowafanya wananchi walipuke kumzomea.
Kitendo hicho kilimfanya diwani huyo atumie muda mwingi kuwalazimisha wananchi wamsikilize bila mafanikio.
Kinana aliamua kumuokoa diwani huyo kwa kumtaka Mkuu wa Wilaya hiyo, Mrisho Gambo, kujibu malalamiko hayo.
Kitendo cha Gambo kusimama na kuanza kujibu, wananchi walilipuka kwa shangwe baada ya kuridhishwa na majibu yake.
Awali wananchi hao, walalamikia kitendo cha halmashauri kutumia
eneo la wananchi kupumzikia katika kituo cha mabasi na kukifanya eneo la
kupaki magari yao.
Akijibu swali hilo Gambo alisema awali wananchi walimpatia
malalamiko ya ukosefu wa choo katika kituo hicho na kwamba sasa kipo na
kuahidi kulifanyia kazi suala hilo ndani ya wiki moja na kituo hicho
kitarudi kwa wananchi.
Aidha Gambo, aliwataka wananchi hao kuendelea kuwasiliana naye juu
ya mambo au matatizo yanayotokea juu yao ili kuyapatia ufumbuzi.
Aidha, alisema pamoja na hatua alizochukua dhidi ya viongozi na
wananchi wanaokiuka sheria na kanuni za nchi ni pamoja na daktari wa
Hospitali ya Maguga ambaye alikuwa akiuza vifaa vya tiba.
Alisema alifuatilia suala hilo na kubaini ukweli hivyo daktari
huyo alikamatwa na kukabidhiwa kwa Takukuru na hadi sasa kesi hiyo
inaendelea.
Pia aliahidi kusimamia suala la walimu kuwafukuza wanafunzi
waliokosa michango mbalimbali ya shule na kwamba mzazi ambaye mtoto wake
atarudishwa aripoti ofisini kwake.
Aidha, wananchi hao walipoulizwa sababu za kumzomea mbunge huyo walisema ni kwa sababu hana msaada kwao.
“Huyu mbunge hana msaada kwetu, Mkuu wa Wilaya, ndiyo amekuwa
akisumbuka na sisi kwa kila tatizo tunalomueleza, kukitokea tatizo
humkosi mkuu wa wilaya lakini mbunge hata kutujulia hali tu hakuna,”
alisema Zaina.
CHANZO:
NIPASHE

إرسال تعليق