MWIMBAJI ADAYA NZINGA WA MALAIKA BAND AFARIKI DUNIA - MASHABIKI WAHOJI KWANINI BENDI IMEENDELEA NA SHOW


MWIMBAJI wa Malaika Band  Adaya Nzinga (wa pili kutoka kulia pichani juu), amefariki dunia Jumapili jioni katika hospitali ya Mwananyamala jijini Dar es Salaam.

Adaya Nzinga alilazwa hapo kwa siku kadhaa, tatizo kubwa ikiwa ni malaria kali iliyopanda kichwani.

Bado haijaelezwa mazishi yatafanyika wapi na lini. Wakati msiba huu unatokea, bendi yake ya Malaika ilikuwa mjini Morogoro katika onyesho la Christian Bella “Nani Kama Mama Tour”.

Mashabiki kadhaa wamehoji juu ya bendi hiyo kuendelea na onyesho wakati msanii wao amefariki.

Mdau mmoja anayekwenda kwa jina la Michael Mpiana Safari ameandika kwenye ukurasa wa facebook wa  rapa wa Malaika ToToo Ze Bingwa:  “Huo ni msiba mkubwa sana hasa kwenu wanamuziki na washabiki pia… sitaki kuamini kama viongozi na wamiliki wa band wametoa ‘go ahead’ ya show kuendelea huku msiba ukitokea kabla ya show kuanza rasmi.

“Najua wamiliki wa band wao wataangalia hasara watakayopata kama wakikatiza hii show kufanyika,, lakini kiutu sio ustaharabu na staha nzuri ya kiafrika kuendelea na burudani huku mwenzenu akiwa amekutwa na umauti....

‘Poleni sana wanamuziki wa Malaika Band kwa kuwa na wakati mgumu sana leo kwa kuomboleza kifo cha mwenzenu wakati huo huo mnatakiwa muwaburudishe washabiki wenu huku wakiwa wametia kilevi kichwani...

Hata hivyo Totoo Ze Bingwa alimfahamisha kuwa kwa vile msiba umetokea jioni huku maandalizi yote ya show yakiwa yamekamilika na ukizingatia kuwa onyesho limekodiwa, basi hawakuwa na namna nyingine zaidi ya kuendelea na show.

Totoo anadai kama msiba ungetokea mapema zaidi, basi wangeahirisha onyesho.

Adaya Nzinga aliitumikia Watoto wa Tembo ya Ndamndaa Cossovo kabla ya kutua Malaika miezi michache iliyopita.

Hisia imeelezwa kuwa katika nyimbo za Malaika zilizoko studio, marehemu Adaya Nzinga ametupia sauti kwenye nyimbo mbili.

Post a Comment

Previous Post Next Post