
Kocha wa Simba Patrick Phiri
Akizungumza na gazeti hili jana kwa njia ya simu, Phiri alisema
Simba ina majeruhi ambao wasingeweza kucheza dhidi ya Yanga katika
tarehe ya awali Oktoba 12, kwenye Uwanja wa Taifa.
"Kwangu ni habari njema," alisema Phiri aliye katika awamu ya tatu
ya uongozi wa benchi la ufundi la Simba alipoulizwa kama kuahirishwa
huko kumeingilia programu yake yoyote. "(Kwa kusogezwa mbele) Sasa Ivo
anaweza akawa amepona mpaka kufikia mchezo huo pamoja na Issa Rashidi na
(Harun) Chanongo.
"Nimepata nafasi ya kuandaa timu ukizingatia mchezo dhidi ya Yanga ni mchezo mkubwa."
Pambano linaloibeba ratiba ya ligi kuu ya Bara la watani wa jadi
hao limeahirishwa na shirikisho la soka (TFF) ili kupisha mchezo wa
kimataifa wa kirafiki baina ya Taifa Stars na Benin siku hiyo.
Wachezaji wanne wa kikosi cha kwanza wa Simba wapo nje kwa sasa na
walitegemewa kuukosa mchezo wa leo dhidi ya Polisi Morogoro na pambano
hilo dhidi ya Yanga mabingwa wa mwaka jana.
Majeruhi hao ni mshambuliaji Paul Kiongera ambaye atakuwa nje ya
uwanja kwa miezi miwili akiuguza goti, golikipa Ivo Mapunda ambaye
ameumia kidole na atakuwa nje kwa wiki mbili. Wengine ni beki Issa
Rashid na Harun Chanongo ambao wanauguza maumivu ya misuli.
Baada ya kusogezwa mbele huko Chanongo, Ivo na Rashid wanaweza kucheza dhidi ya Yanga kwa kuwa wanaendelea kupona.
Wakati huo huo, kocha wa Simba Patrick Phiri amesema timu yake
imepania kushinda leo dhidi ya Polisi kwenye Uwanja wa Taifa baada ya
kuachia uongozi wa mabao mawili na kutoka sare ya 2-2 dhidi ya Coastal
Union Jumapili iliyopita.
CHANZO:
NIPASHE
إرسال تعليق