POLISI nchini Uganda wamekamata kiasi kikubwa cha milipuko walipokuwa wakifanya operesheni ya kutibua jaribio la shambulizi la kigaidi la wanamgambo wa al-Shabab.
Hadi sasa, watu 19 wamekamatwa na Jeshi la Polisi na wanahojiwa kuhusiana na nia yao kutekeleza vitendo vya kigaidi, kulingana na msemaji wa polisi.
Wiki iliyopita, ubalozi ya Marekani mjini Kampala ulionya kuwa kulikuwa na uwezekano wa shambulizi la kulipiza kisasi mauaji wa kiongozi wa kundi hilo la al-Shabab.
Uganda inalaumiwa kwa kutoa majeshi yake kupigana chini ya nembo ya Umoja wa Afrika Amisom.
Marekani ilitangaza kuuawa kwa kiongozi wa kundi la al-Shabab, Ahmed Abdi Godane baada ya shambulizi la angani Septemba 2 mwaka huu.
Serikali inasema kuwa kundi hilo la kigaidi lilikuwa limepanga mashambulizi katika Mji Mkuu wa Kampala.
Askari walisema kuwa kundi hilo lilikuwa limepanga mashambulizi katika miji mingine pia mwishoni mwa wiki.
Jana Jumapili, Marekani iliondoa onyo lao ikidai kuwa iliamini kuwa tishio la shambulizi lilikuwa limeondoka.
Waziri wa Habari nchini Uganda, Rose Namayanja aliwasihi wananchi kuendelea kuwa waangalifu huku serikali ikiendelea kufanya uchunguzi wa mashambulizi yaliyokuwa yamepangwa.
Alisema kuwa watuhumiwa walikuwa wamepatikana na vifaa vinavyohusiana na vitendo vya kigaidi na nia yao ilikuwa wazi sana.
CREDIT: BBC

Post a Comment