POLISI WANASEMAJE KUNANI DODOMA?


Mkazi wa Dodoma akisoma mmoja ya maandishi yaliyosomeka No katiba Ufisadi yaliyo katika Ukuta wa CCM Makao Makuu.

POLISI Mkoani Dodoma inawasaka watu wanaosambaza vipeperushi vya vitisho dhidi ya Wabunge wa bunge maalum la katiba watakaoingia bungeni leo ambapo pia watu hao walichora ukuta wa Jengo la Makao Makuu Chama cha Mapinduzi (CCM).

Vipeperushi hivyo ambavyo vimesambazwa katika maeneo mengi ya Mji ikiwemo CCM, Makao Makuu, maeneo ya Bunge na Uwanja wa Jamhuri. Vilikuwa vikisomeka , ‘Onyo – Dodoma si mahali pa kufuga wezi wa fedha za umma utakayeingia bungeni kuanzia kesho, yatakayokupata utajuta”

Pia katika Jengo la CCM makao makuu na kwenye ukuta wa Uwanja wa Jamhuri kuliandiwa maneno kwa rangi nyekundu yaliyokuwa yakisomeka  No Katiba Ufisadi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), David Misime alisema  jana  alfajiri viliokotwa vipeperushi maeneo mbalimbali mjini Dodoma vyenye ujumbe wa kutishia kuvunjika kwa amani.

Alisema wanaendelea kupokea taarifa za watu wanaodaiwa kuandaa vipeperushi hivyo na wanafanyia kazi ili waweze kuwakamata na kushtakiwa kulingana na kosa walilolitenda hasa la kutoa vitisho na kuhamasisha uvunjifu wa amani.
Kamanda Misime
Kaimu Katibu wa CCM Mkoa wa Dodoma, Dunga Omary akiwaonesha waandishi wa habari (hawapo pichani) moja ya ujumbe wa vitisho kwa wajumbe wa bubnge la katiba vilivyosambazwa jana Mjini Dodoma.

 “ Kila mmoja ajiepushe kujiingiza kwenye kuhamasisha uvunjifu wa amani, kujiingiza katika mikusanyiko isiyo halali na maandamano ambayo yameshapigwa marufuku na Jeshi la Polisi.  Atakayekiuka na kujiingiza katika vitendo hivyo vya kiuhalifu atashurutishwa kwa nguvu zote kwa mujibu wa sheria za Nchi na kwa mamlaka iliyopewa Jeshi la Polisi.” alisema

Pia aliwataka wananchi na wageni wapenda amani waendelee na shughuli zao kama kawaida kwani Jeshi La Polisi limejiimarisha ipasavyo kukabiliana na yeyote yule atakayekiuka sheria na maelekezo yaliyotolewa.

“Inaonekana ni kikundi cha watu kilichoamua kufanya hivyo tutatumia utaalam wetu kuhakikisha kuwa tunawapata” alisema.

 Kwa upande wake, Kaimu Katibu wa CCM Mkoa wa Dodoma, Dunga Omary alisema ni jambo la ajabu kuona kuwa Jengo la CCM linaandikwa maneno kama yale wakati katiba ni ya Watanzania wote.

“ Kwa nini CCM wamelengwa kwani katiba ni ya watanzania hatupaswi kulaumiwa kwa sababu ya katiba” alisema

Alisema ushahidi wa mazingira ya kawaida utaona kuwa wale walioshindwa kuandamana wameamua kufanya hivyo na huko ni kufilisika kisiasa.

“Majuzi chama kimoja cha siasa kilitangaza kufanya maandamano baada ya hilo kushindikana wameamua kufanya mambo hayo huko ni kufilisika kisiasa” alisema

Alisema anaamini Jeshi la Polisi litafanikiwa kuwanasa wale wote waliohusika na kadhia hiyo.

Alisema watanzania ndiyo waamuzi wa katiba lakini isitokee watu wachache.

“hata ukiangalia ujumbe ulio kwenye vitisho una shabihiana na dhamira ya maandamano kwa vile maandamano hayakufanyika wameamua kufikisha ujumbe kwa namna nyingine.

Hata hivyo Kaimu Meneja wa Uwanja wa Jamhuri Saidi Kalela alisema
walipofika kazini jana asubuhi walikuwa ukuta ukiwa umeandikwa No katiba Ufisadi na pia vipeperushi vya vitisho vikiwa vimesambaa eneo hilo.

“Siasa ziwe majukwaani sio kwenye viwanja vya mipira, hapa karibu na uwanja kuna shule mbili wanafunzi wanapita hapa na kuona hali hii nini maana yake, siku nyingine watafute sehemu ya kupeleka vitu visivyo na maana kama hivi sio hapa uwanjani” alisema.
Source:  Sifa Lubasi, habarileoDodoma

Post a Comment

أحدث أقدم