Wadau
mbalimbali wa madini ya vito waliopata bahati kutembelea Banda la
Tanzania katika siku ya kwanza ya Maonesho ya 54 ya Kimataifa ya Vito na
Usonara ya Bangkok, wakishangazwa na mng’ao wa Kito cha Tanzanite
katika Pete iliyovalishwa kidoleni mwa Mwanafunzi, Raia wa Thailand
aliyeomba kujaribisha Pete hiyo. Anayetoa maelezo ni Mfanyabiashara wa
Madini ya Vito kutoka Tanzania, Bw. Gregory Kibusi (Mwenye mavazi ya
Bhatiki).
Sehemu
ya shehena ya madini mbalimbali ya vito katika Banda la Tanzania kwenye
Maonesho ya 54 ya Kimataifa ya Vito na Usonara ya Bangkok.
Mkurugenzi
wa Kitengo cha Uthaminishaji wa Madini ya Almasi na Vito cha Wizara ya
Nishati na Madini – Tanzania (TANSORT), Archard Kalugendo akisalimiana
na Rais wa Taasisi ya Wafanyabiashara wa Madini ya Vito wa Thailand, Bw.
Somchai Phornchindarak baada ya uzinduzi rasmi wa maonesho hayo.
Na Veronica Simba – Bangkok
Banda la Tanzania katika siku ya
kwanza ya Maonesho ya 54 ya Kimataifa ya Vito na Usonara ya Bangkok,
yaliyozinduliwa Septemba 9, 2014 nchini Thailand, limekuwa na mvuto wa
kipekee kwa wadau wa madini husika kutoka mataifa mbalimbali duniani
waliofika katika maonesho hayo.
Mkuu wa Banda la Tanzania, ambaye
pia ni Mkurugenzi wa Kitengo cha Uthaminishaji wa Madini ya Almasi na
Vito cha Wizara ya Nishati na Madini (TANSORT), Archard Kalugendo
alisema, wadau wengi waliofika katika maonesho hayo, walivutwa na aina
mbalimbali za madini ya vito yanayopatikana Tanzania hususan Tanzanite.
“Unajua, Tanzanite ni madini
yanayopatikana Tanzania pekee ambapo sifa hii inayafanya kuwa madini
yenye mvuto wa pekee,” alisema Kalugendo.
Aliongeza kuwa, mbali na kuwa
Tanzanite inapatikana Tanzania pekee, lakini pia ina mvuto wa pekee
machoni mwa watazamaji ambayo ni sababu nyingine inayowavutia watu wengi
kupenda kufahamu zaidi kuhusu madini hayo, hali ambayo imesababisha
watu wengi kutembelea Banda la Tanzania.
Alifafanua kuwa, pamoja na kuwepo
mabanda kutoka nchi nyingine yaliyo na madini ya Tanzanite katika
maonesho hayo, wengi wa wadau walitembelea Banda la Tanzania wakitaka
kuelimishwa zaidi kuhusu madini hayo, hali inayodhihirisha kuwa ufahamu
kwamba Tanzanite inatoka Tanzania pekee umeongezeka kwa watu kutoka
mataifa mbalimbali.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti,
Wafanyabiashara wa Madini ya Vito kutoka Tanzania wanaoshiriki katika
maonesho hayo, Gregory Kibusi na Kassim Pazi walisema ushiriki wa
Tanzania katika maonesho husika kwa msimu huu umeboreka zaidi kutokana
na maandalizi mazuri yaliyofanyika.
“Tulitumia uzoefu tulioupata
katika maonesho ya msimu uliopita na hivyo tukajipanga vizuri zaidi
kuhakikisha tunakuwa na ushiriki wenye tija msimu huu na ndiyo maana
katika siku ya kwanza tu ya maonesho, tumeshuhudia banda letu
likitembelewa na watu wengi sana,” alisema Kibusi.
Naye Gregory alifafanua kuwa
maandalizi waliyofanya ni pamoja na kuandaa madini ya kutosha hasa yale
yaliyokatwa tayari, ambayo ndiyo yanayopendwa zaidi na wadau wengi
wanaofika katika maonesho.
Kwa upande wake, Mtaalamu wa
Madini ya Vito kutoka TANSORT, ambao ndiyo waratibu na wasimamizi wa
ushiriki wa Tanzania katika maonesho hayo, Teddy Goliama alisema
maandalizi mengine yaliyofanyika ni pamoja na kuwepo na washiriki wengi
zaidi wakijumuisha wachimbaji na wafanyabiashara wa madini husika pamoja
na maafisa kutoka Wizarani.
Vilevile alisema kuwa, mbali na
kutangaza madini mbalimbali yaliyopo Tanzania, Ujumbe wa Tanzania
unaoshiriki katika maonesho hayo unafanya kazi ya kuitangaza nchi kwa
ujumla ikiwa ni pamoja na fursa mbalimbali za uwekezaji pamoja na
vivutio vya utalii.
“Tumeamua kutumia fursa hii ya
maonesho kuitangaza nchi kwa ujumla. Tunawashukuru Wizara ya Maliasili
na Utalii kupitia Bodi ya Utalii ambao walitupatia vipeperushi, picha za
video na makabrasha mbalimbali yenye kutangaza vivutio vya utalii wa
nchi yetu. Tumegawa vipeperushi vingi ambavyo tunaamini vitasaidia sana
kuitangaza nchi yetu katika anga za kimataifa na hivyo kuvutia watalii
na wawekezaji wengi zaidi,” alisema Teddy.
Maonesho ya 54 ya Kimataifa ya
Vito na Usonara ya Bangkok, yaliyofunguliwa Septemba 9 mwaka huu na
Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara ya Thailand, Bi. Chutima
Bunyapraphasara, yanatarajiwa kuhitimishwa Septemba 13, 2014. Hii ni
mara ya pili kwa Tanzania kushiriki maonesho hayo.

إرسال تعليق