Na Freddy Macha
Jumatano ijayo tarehe 15 Oktoba, 2014...kundi la kina mama watatu
akiwemo Mtanzania litashiriki jopo la ukeketaji na Wabunge, London,
Uingereza.
Mtanzania, Rhobi Samwelly, mama wa watoto wanne, ni mzawa wa
Butiama, Mara. Wenzake ni Comfort Momoh, toka Nigeria, anayetibu
wanawake waliokeketwa hospitali mbili za Guy’s na St Thomas, London
na Ann-Marie Wilson mkurugenzi wa “28 Too Many.” Shirika hili lenye
tovuti yenye http://28toomany.org/ ni maktaba kubwa yenye habari,
picha, utafiti na uchunguzi wa ukeketaji duniani.
Bango linalotumika kuchangia makutano na hafla mbalimbali za fedha za ujenzi wa nyumba ya hifadhi ya wasichana Mugumu, Mara |
Mwaka1997 Comfort Momoh alianzisha msururu wa shughuli za
kuwasaidia akina mama waliokeketwa likiwemo shirika la African Well
Women’s Clinic. Bi Momoh mwenye shahada ya uzamili (MA) ni mshauri
wa shirika la Afya duniani (WHO) kuhusu adha ya ukeketaji.
Mtanzania Rhobi na Ann-Marie walikuwa baadhi ya wazungumzaji
kwenye hafla iliyofanywa Alhamisi na Jumamosi iliyopita kuchanga
fedha za kujenga nyumba ya hifadhi kwa wasichana wanaokimbia
ukeketaji, Mugumu, Mara.
Hafla hiyo iliendeshwa na shirika la urafiki baina ya Tanzania na
Uingereza (British Tanzania Society) na Shirika la Misaada ya
Kimaendeleo Tanzania (Tanzania Development Trust Fund). Fedha
zilizokusanywa zinaendelea kusaidia ujenzi wa nyumba ya kuwahifadhi
wasichana wanaokimbia ukeketaji jimbo la Mara.
Mwanasaikolojia, mtafiti na mtetezi wa haki za waliokeketwa, Anne-Marie Wilson(kulia kabisa) akijadiliana na wanachama wengine wa Jumuiya ya Uingereza na Tanzania (BTs), ukumbi wa Central Hall, Westminster baada ya hotuba yake. Alisisitiza kila sekunde kumi , msichana fulani hukeketwa ulimwenguni. Kati kati ni mweka hazina wa BTs, Bw. Robert Gibson na Jonathan Cape, mwendeshaji wa hafla. |
Nilimuuliza Dada Rhobi je hawa wasichana hawatadhurika? Je, wazazi
husika hawatawafuata? Akajibu kwa sasa kuna vyombo vingi husika
kikiwepo polisi, serikali na kanisa la Anglican ambalo yeye ni mjumbe
pia.
Rhobi ni mratibu wa shughuli mbalimbali za kimaendeleo ya akina
mama vijiji vya Mara. Mbali na ukeketaji anaangalia pia maslahi ya
unyanyasaji wa kijinsia. Baada ya Bi Neema Wambura kupigwa na
mumewe majuma kadhaa yaliyopita, Bi Rhobi alikuwa mmoja wa
waliomhudumia kwa kuhakikisha anapata matibabu. Neema alimwagiwa
maji moto na kuunguzwa kifuani na mkononi.
Kufuatana na maelezo ya dada Rhobi na Ann-Marie leo hii wastani wa
wasichana wanaokeketwa ni miaka minane hadi kumi na nne. Ila wapo
wazazi wanaowapeleka watoto wenye miaka miwili.
Nchi 29 duniani ikiwemo Tanzania bado zinakeketa wasichana. Licha
ya kufanywa vilema, kujifungua kwa shida, kupata maumivu ya daima
wakati wa haja ndogo na hedhi, baadhi ya wasichana hufa.
Dada Rhobi Samwelly: “Msichana anapokufa mwili hutupwa tu
vichakani na kuliwa na wanyama. Huwa siri. Wanaficha. Mama aliyefiwa
huwambiwa asilie, asiwaambie watu. Ni aibu. Asiomboleze. Asilie. Ni
mkosi. Balaa.”
Kawaida kipindi cha ukeketaji ni miezi ya Novemba na Desemba, kila
miaka miwili. Wasichana wanaokimbia adha hii wamekuwa wakilindwa
na kanisa na sehemu nyingine. Yumkini nyumba inayojengwa Mugumu
itakuwa mkombozi wao. Gharama zake zimekadiriwa kuwa takribani
paundi 60, 000 za Uingereza. Paundi moja na shilingi elfu mbili na kitu.
Ukeketaji ambao unajulikana dunia nzima kwa jina FGM (female genital
mutilation) huwa wa aina nne. Aina iliyoenea ni kuondoa kinembe,
kuondoa midomo ya uke, tatu kuondoa kinembe na midomo. Aina hizi
tatu za kukeketa zina lengo za kupungusa kabisa hisia za ngono na
mapenzi ya mwanamke. Desturi iliwekwa ili wanawake wasitembee ovyo
nje ya ndoa, wawe tu wazazi na mali za waume zao. Ya nne ni kuondoa
kila kitu na kubakisha tundu la haja ndogo na mfereji wa damu siku za
hedhi.
Mwanamke anapojifungua hupasuliwa akishamaliza hushonwa tena.
Utaratibu huo huendelea maisha yake yote ya uzazi. Wanawake husika
hutembea na maumivu usiku na mchana maisha yao yote. Ngono,
mapenzi, uzazi vyote si furaha kwao.
Si kweli ukeketaji ni suala la dini. Ulikuwepo kabla ya dini tunazofuata
toka Mashariki ya Kati zilipoingia.
Moja ya kazi za muuguzi Comfort Momoh ni kusaidia wanawake hawa.
Licha ya nchi 29 za Kiafrika, Mashariki ya Kati na bara Asia, nchi za
Kizungu za Ulaya, Marekani, Canada na Australia pia zinao wahamiaji
wanaoendesha shughuli hizi. Kisheria ukeketaji unakatazwa lakini
utekelezaji haujawa makini.
Mwezi Juni, Kamishna wa Haki za Binadamu, Umoja wa Mataifa Navi
Pillay alisisitiza ukeketaji hauna faida zozote za kiafya. Ukeketaji
alifafanua Bi Pillay, “unaathiri maisha na kuhatarisha maisha ya watoto
waliozaliwa na kina mama walioupitia.”
Bi Pillay alisisitiza kwamba vita au mapambano dhidi ya ukeketaji ni
kazi yetu sote wanaume, wanawake, watoto, vijana kwa wazee.Bila
kuchagua umri, jinsia au rangi.
Jopo la Jumatano, Bungeni Uingereza, litakuwa chini ya uenyekiti wa
Mbunge wa Jimbo la Stafford, Jeremy Lefroy, ambaye anawakilisha
chama cha Conservatives. Bwana Lefroy pia huendesha shirika la
ufadhili wa maendeleo Equity Africa lenye dhamira ya kupunguza
umaskini barani.
Wazungumzaji wengine ni Lynne Featherstone, Mbunge
anayewakilisha serikali kwa ajili ya shirika la Kimaendeleo ya Kimataifa
Uingereza (DFID).Mwaka jana DFID ilijitolea kiasi cha paundi 35 milioni
kupunguza ukeketaji duniani kwa asilimia 30.
-London, 10 Oktoba 2014.
-Bpepe: kilimanjaro1967@hotmail.com
-Tovuti: www.freddymacha.com
Anna Marcus, wa Jumuiya ya Uingereza na Tanzania (BTs) akishangilia bendera za
Tanzania.
Janet Chapman & Jonathan Cape Waingereza wanaojali maendeleo ya Watanzania.
Wameendesha maonyesho matatu mwaka huu mjini London, kusaidia mchango wa fedha
za ujenzi wa nyumba ya hifadhi ya wasichana wanaokimbia ukeketaji , Mugumu, Mara.
Mheshimiwa Jeremy Lefroy, Mbunge wa jimbo la Stafford, Uingereza. Atasimamia jopo la
Jumatano ijayo. Picha toka tovuti yake.
Bi Rhobi Samwelly (katikati) akiwa na mkewe Balozi wetu Uingereza, Mama Joyce
Kallaghe(kushoto) na Bi. Mariam Kilumanga, mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake wa
Tanzania, Uingereza (TAMWA). Hafla ya kukusanya fedha kusaidia ujenzi wa kituo cha
wasichana wanaokimbia ukeketaji Mugumu, Mara.
Rhobi akiwa na Fahma (kushoto) mzungumzaji mwingine toka Afrika aliyekemea Ukeketaji.
Wasikilizaji wa kilichokuwa kikiongelewa. Pichani ni Tony Janes aliyefanya kazi Tanzania
miaka ya zamani. Siku hizi kastaafu.
Post a Comment