Mahojiano na Bosire Boniface huko Garissa
Mwandishi wa Somalia Abdisaid Abdi Ismail amekuwa katika uchunguzi mkali
baada ya kuchapisha kitabu kilichoandikwa kwa lugha ya Kisomali chenye
jina "Sheria ya Uasi dini katika Uislamu: Je ni sahihi?" ambapo ametoa
hoja kwamba hakuna uhalalishaji wa kidini wa mauaji ya watu kwa sababu
ya kuasi dini.
Mkaazi wa Garissa akiwa na nakala ya
kitabu "Xadka Riddada Maxaa Ka Run Ah?" ("Sheria ya Kuritadi katika
Uslamu: Je ni Sahihi?") tarehe 24 Oktoba, 2014. [Bosire Boniface/Sabahi]
Kitabu hicho kimeibua majibu mchanganyiko miongoni mwa jamii ya Kisomali
nchini Kenya na Somalia kufuatia uzinduzi wake huko Nairobi tarehe 14
Septemba.
Baada ya maulamaa kadhaa kutoa wito wa kitabu hicho kupigwa marufuku na
kuchomwa, Maduka mengi ya kuuza vitabu ya Wasomali huko Eastleigh
yameacha kuuza kitabu hicho, na sasa kinauzwa "kwa tahadhari" katika
maduka machache ya kuuza vitabu huko Garissa na Nairobi na pia kupitia
mtandao, Ismail alisema.
Ismail, raia wa Galkayo mwenye umri wa miaka 50 alipata udhamini wa
masomo kutoka chuo kikuu cha Umm al-Qura huko Mecca, Saudi Arabia,
ambapo alisoma sheria ya didni na uraghibishi, alihitimu 2002 shahada ya
uzamili katika masuala ya uchumi wa Uislamu. Kutokea hapo, Ismail
ameandika vitabu viwili kwa Kiarabu, "Nchi za Kiislamu' Kuongeza Mtaziko
wa Madeni" na "Dunia kuwa kijiji kimoja katika Dunia ya Kislamu: Ukweli
na Takwimu", na vitabu vingine viwili kwa Kisomali, "Saboolnimada sidee
looga baxaa?" na "Hordhaca Dhaqaala Islaamka".
Ismail, baba wa watoto watatu, anafundisha uchumi katika chuo kikuu cha
Afrika Mashariki huko Bosaso tangu 2009, lakini amesema hawezi kurudi
Somalia sasa kwa vitisho vya kifo ambavyo amekuwa akipokea kutoka
alipochapisha kitabu hicho kipya huko Nairobi.
Katika mahojiano ya kina na Sabahi, Ismail alizungumza juu ya umuhimu wa
kujadili mada ya uasi dini katika Uislamu, utafiti wake kuhusu mada
hii, na umuhimu wa kuhamasisha na kuhimili mjadala wenye tija kuhusu
mawazo tofauti miongoni mwa Wasomali.
Sabahi: Tuambie zaidi kuhusu kitabu chako na kwa nini ulikiandika.
Abdisaid Abdi Ismail: Mawazo makuu ya kitabu hiki ni kuhusu uasi dini
katika Uislamu, lakini pia kinazungumza kuhusu masuala mengine kadhaa
kama vile dola na dini, usawa wa kijinsia kulingana na fedha zinazolipwa
fidia kwa familia ya mtu aliyeuawa, kifo kwa kuwapiga mawe wanaume na
wanawake wazinifu, na kadhalika.
Niliandika kitabu hiki kwa jamii ya Wasomali kuwafanya wajue baadhi ya
masuala muhimu katika dini yao ambayo yanahusisha maisha yao katika
dunia hii na baada ya hapo, ambayo baadhi ya Maulamaa wa Kisomali
wamekuwa wakieleza mara kwa mara kwa namna ambayo haiendani na maana
halisi ya mafundisho ya Kiislamu.
Ni matumaini yangu kwamba anayesoma kitabu hiki atagundua kinachosemwa
na Uislamu kuhusu masuala yaliyozungumziwa katika kitabu hiki, lakini
ujumbe muhimu ni kwamba Uislamu ni dini inayojali ubinadamu na msamaha,
na maadili yake yanahusu maisha ya binadamu.
Sabahi: Umefanya suala la kuritadi kuwa lengo kuu. Kwa nini unafikiri ni muhimu sana kwa sasa na muhimu kwa Wasomali kuelewa?
Ismail: Ni suala muhimu sana katika jamii ya [Uislamu] leo hii kwa
sababu vikundi vya wenye msimamo mkali vinatumia suala la uasi wa dini
kama nyenzo ya kuhalalisha mauaji yao ya kutisha na ya kikatili dhidi ya
wale wanaopinga tafsiri yao yenye makosa ya Uislamu au hata ajenda yao
ya kisiasa.
Suala hili ni muhimu sana kwa jamii ya Kiislamu kwa ujumla, lakini hasa
kwa jamii ya Somalia, kwa sababu damu yao inamwagwa kila siku kwa
kutumia uasi wa dini kama nyenzo ya kulihalalisha.
Nafikiri mada inastahili kujadiliwa katika namna pana katika hali ya
sasa ya ulimwengu wa Kiislamu. Ningependa kama mtu mwingine angeweza
kuandika kuhusu hilo, lakini bahati mbaya hakuna aliyeandika kuhusu hilo
na hilo limenilazimisha kufanya hivyo sasa, na ninachagua lugha ya
Kisomali ili niweze kuwafikia watu wanaozungumza Kisomali Afrika
Mashariki na duniani kote kwa ujumla.
Sabahi: Je, kifo ni adhabu inayofaa kwa kuritadi na kulingana na mafundisho ya Kiislamu?
Ismail: Nimekuwa nikifanyia utafiti suala la kuritadi kwa kipindi kirefu
sasa, nikilinganisha mitazamo mbalimbali na ushahidi ambao kila kikundi
cha msimamo mkali kinautumia na Korani na mafundisho ya mtume
yanasemaje kuhusu hilo.
Kilichofanya ugunduzi wangu kuhitimishwa ni kwamba adhabu ya kifo kwa
uasi wa dini haina hoja yoyote ya halali katika Uislamu ingawaje imekuwa
ikitumika kwa karne nyingi kwa madhumuni ya kisiasa kwa wasomi
wanaotawala katika msururu wa utawala wa kihistoria wa Uislamu kama njia
ya uhaini kwa Waislamu ambao wanaacha dini, kwa sababu dini ilikuwa
utambulisho wa pamoja kwa watu wakati huo.
Sabahi: Je, utafiti wako unasema adhabu sahihi ni ipi kwa uasi wa dini kwa mujibu wa Uislamu?
Ismail: Kwa kuzingatia uhakiki wa wanazuoni wa mafundisho ya dini, maoni
yangu kuhusiana na uasi wa dini ni kwamba hakuna adhabu ya uasi wa dini
katika ulimwengu huu. Adhabu iko katika maisha ya mbinguni na ni kati
ya mtu na Mungu.
Uhuru wa dini na imani ni baadhi ya haki za msingi za binadamu na hakuna
mtu mwenye haki ya kuingilia kile ambacho wengine wanaamini. Mawazo na
maoni tofauti na mbalimbali ni muhimu sana kwa kuishi pamoja, kuelewana
na maendeleo ya jamii yoyote.
Sabahi: Kwa nini Waislamu wanapaswa kusoma kitabu hiki?
Ismail: Wanapaswa kukisoma kwa sababu wanahitaji kujua ukosefu wa
uhalali halisi kwa adhabu ya uasi wa dini katika Uislamu, ambao
nimeridhika kwamba hakuna uungaji mkono halali kuruhusu adhabu ya kifo
kwa uasi wa dini katika Uislamu.
Kitabu kitafafanua kwa wasomaji masuala mengine mengi moja kwa moja au
isivyo dhahiri kuhusiana na suala la uasi wa dini na inategemewa
kitashawishi vikundi kuacha kutumia [suala hili] kuua watu [kwa
kuzingatia] uhalalishaji wa kupotosha.
Ninatumaini kwamba wakati [idadi ya] watu wanaosoma kitabu inaongezeka,
uendawazimu unayoikumba nchi yetu utapungua kidogo na hatimaye vijana
watatambua kuwa wanatumiwa dhidi ya watu wao chini ya kisingizio cha
kutokuwa Waislamu.
Sabahi: Kitu gani kinakosekana katika mazungumzo miongoni mwa Wasomali wanapojadili masuala na mawazo haya?
Ismail: Vipengele kadhaa vinakosekana katikajambo hili, kama vile
kufikiria kwa kina na wanazuoni wapya ambao wanaweza kutafsiri Kuran na
hadithi (mafundisho ya Mtume Mohammed) kwa mujibu wa muktadha wake wa
asili bila ya upendeleo wa vikundi mahususi ambavyo vinataka kuuteka
Uislamu kwa manufaa yao wenyewe.
Kunatakiwa kuwa na mazungumzo ya wazi na huru miongoni mwa wanazuoni na
ujumbe wa namna ya kutafsiri vyanzo vya Kiislamu katika njia ambayo
inaweza kusaidia Waislamu kuishi kistaarabu na kwa uvumilivu kama
wanavyopaswa kuishi, ili iwawezeshe kuishi kwa amani miongoni mwao
wenyewe na wengine katika dunia yetuu hii.
Sabahi: Je, nini ni chanzo cha itikadi ya al-Shabaab?
Ismail: Ninaamini kwamba al-Shabaab na vikundi vingine vinavyofanana na
hicho wanatekeleza tu mafundisho na uelewa wa baadhi ya wanazuoni wa
kiislamu ambao wanatafsiri baadhi ya vifungu vya kiislamu kwa mujibu wa
ajenda zao.
Kupata uelewa wa al-Shabaab na wenye msimamo mkali wengine, kwanza
tunapaswa kufafania Kuran na masimulizi na vyanzo vingine vya Kiislamu
kutokana na maandiko yake halisia. Vita dhidi ya al-Shabaab na wengine
wenye msimamo mkali ni vita vya mioyo na akili za jamii ya Kiislamu na
kuvishinda vita hivyo tunapaswa kurejea hali halisi ya Uislamu ambayo ni
ya amani, uvumilivu na ya kidemokrasia.
Sabahi: Vikundi kama vile al-Shabaab wanadai kujaribu kuunda jamii
halisi kama ilivyokuwa wakati wa Mtume Mohammed. Je, ni kipi kibaya kwa
kufanya hivyo?
Ismail: Hakuna lililo baya, lakini ni nani anayewasilisha hilo? Hoja
langu ni kwamba tunatakiwa kuelewa Uislamu halisi, na sio Uislamu wa
kisiasa.
Kwa upande mwingine, tunapaswa kuzingatia tofauti kati ya kipindi
ambacho Mtume Mohammed, amani iwe juu yake, na alioishi nao wakati huo,
na dunia yetu, katika karne ya 21, wakati hali ya maisha ni tofauti
kabisa.
Sabahi: Je,ulitarajia majibu hasi kwa kitabu chako?
Ismail: Kwa kweli, nilitarajia kitabu hiki kuanzisha mjadala wa
kitaaluma miongoni mwa wanazuoni, lakini kamwe sikutarajia kwamba mtu
fulani atatoa wito wa kukizuia kitabu hicho na kutangaza kuwa mwandisi
ni muasi wa dini.
Hilo ndilo jambo ambalo kitabu hiki kinajaribu kuzungumzia na inaonekana
wale waliopo katika msimamo mkali hawakuelewa kabisa ujumbe mkuu wa
kitabu hicho, ambao ni [kuhamasisha] mazungumzo na mjadala.
Hata hivyo, kumekuwa na majibu chanya kutoka kwa watu mbalimbali ambao wanasema muda ulikuwa sahihi kuibua suala hilo.
Sabahi: Je, unafanyaje na nini kitakachofuata kwako?
Ismail: Nilikuja Nairobi kutoka Somalia mwezi Agosti mwaka huu kwa lengo
la kuchapisha kitabu hiki kwa kuwa hakuna wachapishaji nchini Somalia.
Kama kungekuwa na wachapishaji nchini Somalia, hata hivyo wasingekuwa
tayari kuchapisha kitabu hiki.
Sasa ninajaribu kujiokoa kutoka kwa baadhi ya watu wenye itikadi kali na
wafuasi wao ambao hawajazificha nia zao za kunidhuru badala ya kitabu
changu. Mienendo yangu ni ya siri na imepunguzwa, mara nyingi ninakuwa
ndani ya nyumba.
Wakati huo huo, ninaaandika kitabu kingine kinachousu namna Uislamu wa
amani unavyoweza kusambazwa miongoni mwa jamii ya Somalia. Sitazuiliwa
wala kutishwa kutokana na mazungumzo na kujadili masuala ambayo ninaona
ni muhimu kuleta Uislamu halisi na sahihi kwa jamii nyingi. Nitaendelea
kurejelea ukweli kuhusu msimamo sahihi wa dini kuhusu masuala kadhaa
ambayo nimeyazungumzia katika kitabu hiki na [masuala] mengine.
Chanzo: sabahionline.com
Post a Comment