Breaking News:- Miss Tanzania 2014, Sitti Abbas Mtemvu Ajivua Taji!

Miss Tanzania 2014 Sitti Abbas Mtemvu ajivua taji
Katika hatua ambayo pengine ilitarajiwa na wengi, mshindi wa taji la Miss Tanzania mwaka 2014, Sitti Abbas Mtemvu, amejivua taji hilo “aliloshinda” wiki mbili  zilizopita. Uamuzi wa Sitti ambaye ni mtoto wa Mbunge wa Temeke, Abbas Mtemvu, unakuja baada ya gharika ya maoni mbalimbali na ushahidi ulioonyesha kwamba kuna utata mkubwa katika suala zima la umri wake. Pia kulikuwepo na tuhuma za yeye kuwa na mtoto kitu ambacho ni kinyume na vigezo vya kushiriki  shindano hilo ambalo kwa kiasi kikubwa limeendelea kupoteza maana mwaka baada ya mwaka.
Kama ambavyo watu wengi wamekuwa wakifanya katika siku za karibuni, Sitti ametangaza uamuzi wake muda mfupi uliopita kupitia mtandao wa kijamii wa Facebook kwa kuandika ujumbe huu;
HABARI ZA JIONI WATANZANIA WENZANGU, KUTOKANA NA KUWA NIMEKUWA NIKISEMWA SANA, MANENO MENGI YASIO NA TIJA JUU YA HILI TAJI LA UMISS TANZANIA 2014,,,MPAKA KUPELEKEA NISIWE NA AMANI NA UHURU NDANI YA NCHI YANGU TANZANIA, KWA ROHO SAFI NIMEAMUA MWENYEWE KUJIVUA TAJI HILO NA KUACHA WANAYE ONA ANASTAHILI TAJI HILI APEWE ILI NIENDELEE NA MAISHA YANGU KWA AMANI ,ISIWE SHIDA SANA KWANI SITEGEMEI TAJI HILI ILI KUISHI!!
Kimsingi BC tunaamini kwamba uamuzi wa Sitti sio tu kwamba ni wa busara bali pia ulikuwa hauepukiki. Pia hili ni funzo zuri kwa watu kama Kamati Ya Miss Tanzania kutambua kwamba tunaishi katika zama tofauti. Ni zama za utandawazi unaokwenda sambasamba na tekinolojia za hali ya juu kitu ambacho  kinafanya sio tu mazingira ya usiri kuwa magumu bali pia wananchi wa kawaida wana nguvu ya kutoa madukuduku na maoni yao.

Post a Comment

Previous Post Next Post