IKULU YALIJIBU TUHUMA ZA MWEKEZAJI WA MRADI WA RELI - PUGU - DAR



TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Gazeti la Raia Mwema la wiki hii ya Oktoba 8-14 ambalo limetolewa juzi, Jumatano, Oktoba 8, 2014, limeandika kwenye ukurasa wake wa kwanza habari yenye kichwa cha habari, “Mwekezaji aliyemzawadia saa Kikwete aibua utata”.

Kichwa cha habari hicho kinafuatiwa na habari yenyewe ambayo kwenye moja ya aya zake inadai kuwa “tayari Rais Kikwete amekutana na mwekezaji huyo wa Marekani, Bwana Roberk Shumake na kumpa zawadi ya saa aina ya Rolex katika mojawapo ya ziara za Rais nchini Marekani”.
Hii ni habari ya uongo na haiwezi kuwa ya uongo zaidi kuliko 


ilivyochapishwa.

Ni habari ya uzushi na upuuzi. Ni habari inayolenga kumdhalilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete kwamba amepokea zawadi kutoka kwa mtu ambaye anajaribu kupewa kandarasi kujenga usafiri wa treni jijini DSM na ambaye pia anahusishwa kwenye shughuli nyingine za kibiashara zenye utata huko kwao Marekani. Rais Kikwete hakuwahi kupewa wala kupokea saa ya aina ya Rolex kutoka kwa Bwana Shumake ama kutoka kwa mfanyabiashara mwingine yoyote.
Alichopewa Mhe. Rais na Balozi huyo wa Heshima anayewakilisha Tanzania katika jimbo la Michigan ni saa ya kumbukumbu ya mji wa Detroit ambako ndiko nyumbani kwa Bw. Shumake (Souvenir watch), sio saa ya aina ya Rolex kwa matumizi binafsi ya Mhe. Rais. Saa hiyo ya kumbukumbu ni mali ya Tanzania.
Na wala siyo hulka wala tabia yake ya kupokea zawadi kutoka kwa watu wanaotafuta fursa za kuwekeza katika Tanzania. Isitoshe kwa nafasi yake kama Rais hahitaji kupewa saa na watu wa nje kwa sababu mahitaji yake yote ya mavazi na mengine hutolewa kwake na Taifa analoliongoza.
Ni jambo la kusikitisha sana kuwa gazeti la hapa nyumbani linaweza, bila ushahidi wowote na kwa kukariri habari kutoka kwenye mitandao ya kijamii, kuamua kuchapisha habari yenye kulenga kumdhalilisha kiongozi wa Taifa letu, tena kwa kumhusisha na zawadi ya kipuuzi kama saa aina ya Rolex.
Ni matarajio yetu kuwa Gazeti hilo litaombwa kutoa ushahidi wa habari hiyo, ili kuondoa utata ambao dhahiri utajitokeza kutokana na kuchapishwa kwa habari hiyo.
Imetolewa na; Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
9 Oktoba, 2014.

Post a Comment

Previous Post Next Post