Rais
Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akizungumza na mabalozi wa Afrika
wanaoziwakilkisha nchi zao nchini China wakati alipokutana nao jijini
Beijing China leo asubuhi.Raius Kikwete yupo nchini China kwa ziara ya
kiserikali.(picha na Freddy Maro).
. Unatoa nafasi kwa nchi kupata mawazo na fikra mpya
.Anaamini Tanzania itapata Rais bora zaidi wa kumrithi yeye
. Atamani muda wake umalizike akalee wajukuu
Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
amesema kuwa mfumo wa Tanzania ambako Rais anatumikia nafasi ya uongozi
kwa muhula wa miaka mitano na siyo zaidi ya miaka 10 ni mfumo mzuri na
unaovutia kwa sababu unaiwezesha nchi kupata fikra na mawazo mapya.
Aidha, Rais
Kikwete amesema kuwa anaamini kuwa Tanzania itapata Rais bora zaidi
kuliko yeye, Rais ambaye ataiwezesha Tanzania kusonga mbele kwa kasi
kubwa zaidi.
Rais
Kikwete pia amesema kuwa anayo hamu kubwa ya kumaliza muda wake wa
uongozi, ili arudi kijijini kushughulika na wajuu wake na mifugo yake.
Rais
Kikwete ametoa kauli hiyo jana, Jumatano, Oktoba 22, 2014, mjini
Beijing, China, wakati akizungumza na mabalozi wa Afrika
wanaoziwakilisha nchi zao katika China.
Mkutano huo
uliofanyika kwenye Nyumba ya Kufikia Wageni wa Serikali ya China ya
Diaoyutai, ulikuwa shughuli ya kwanza ya Rais Kikwete katika ziara yake
rasmi ya siku sita ya Jamhuri ya Watu wa China ambako amealikwa na Rais
Xi Jinping.
Wakati wa
maswali na majibu, Mheshimiwa Balozi Sola Onadipe, Naibu Balozi wa
Nigeria katika China, alishangazwa na kauli ya Rais Kikwete kuwa
anatamani amalize muda wake wa uongozi, ili astaafu na kusema kuwa
lingekuwa jambo la maana kwa Afrika kama viongozi wengine wangekuwa na
mawazo ya namna hiyo ya kuheshimu Katiba za nchi zao na kung’atuka
kwenye uongozi muda wao unapowadia.
Rais Kikwete amemwambia Balozi huyo: ”
Ni kweli naona kama muda hauendi kwa kasi ya kutosha, ili niweze kuwa
raia wa kawaida na nipate muda wa kuchunga ng’ombe na mbuzi wangu na
nilime mananasi yangu kwa nafasi ya kutosha. Lakini Mheshimiwa Balozi
usishangazwe na utayari wangu kuondoka katika uongozi.”
“Kwanza
utaratibu huu wa miaka mitano ama miaka 10 ni utaratibu wa Kikatiba, ni
jambo lililoko katika Katiba yetu na hatuna kishawishi cha
kulibadilisha. Pili, kazi hii ya Urais ni kazi ngumu sana. Kwa hakika,
binafsi nawaonea gele sana wenye nguvu na ubavu wa kutaka kubakia kwenye
kazi hii kwa miaka mingi. Pengine wana nguvu zaidi kuliko mimi,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“
Lakini pia kuna uzuri katika mfumo huu wa kwetu kwa sababu kila baada
ya miaka mitano na hata kama ni baada ya kila miaka kumi, anaingia mtu
mwingine madarakani akiwa na fikra mpya na mawazo mapya.”
“
Mfumo huu ni mfumo unaoniridhisha sana na wala hakuna kinachonishawishi
nibakie katika madaraka zaidi ya muda wangu kikatiba. Nina hakika, nchi
yetu itapata kiongozi mwingine, bora kuliko hata mimi, kuongoza vizuri
nchi yetu.”
Rais
Kikwete pia amesema kuwa siyo busara pia kwa kiongozi kuwasikiliza wale
wanaoshauri wakisema kuwa akiondoka madarakani nchi itavurugika.
“Kwa
hakika, hawa wanatetea maslahi yao tu wakisema kuwa ukiondoka wewe
madarakani, wao hawatakuwa tena mabalozi ama mawaziri ama nafasi
nyingine yoyote.”
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
22 Oktoba, 2014
Post a Comment