Naibu
Waziri wa Maji, Mhe. Amos Makalla na Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Subira
Mgalu wakiwa wamesimama kwenye mashine ya kuchimbia visima iliyonunuliwa
na Halmashauri ya Wilaya ya Muheza kwa takribani Sh. Mil 240.
Naibu Waziri wa Maji, Mh. Amos
Makalla ameahidi Sh. Milioni 500 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya
maji kwa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza.
Mhe. Makalla alitoa kauli hiyo
jana, alipotembelea Wilaya hiyo kukagua utekelezaji wa miradi ya maji na
hali ya huduma ya maji wilayani humo.
“Nawapongeza sana Halmashauri
yenu na uongozi wake kwa kununua mashine kwa ajili ya kuchimba visima
vya maji, sijawahi kutembelea Wilaya yoyote nchini nikakuta jambo hili.
Kitendo cha Halmashauri kukusanya mapato yake na kufanya hivi,
mnastahili pongezi na kuwa mfano kwa Halmashauri nyingine nchini,”
alisema Makalla.
“Nimeridhishwa na jitahada zenu na
nitahakikisha mnapata mgao wa Sh. Milioni 500 ili kufanikisha lengo la
kupatia ufumbuzi tatizo la maji Muheza,” aliongeza Makalla.
Naibu Waziri alisema kwamba kama
kiongozi mwenye dhamana kwenye Serikali Kuu, atahimiza maamuzi yafanyike
upesi ili jitihada zinazofanywa na Wilaya ya Muheza zifikie lengo
walilojiwekea kuwapatia wananchi maji.
Aidha, Naibu Waziri wa Maji, Mh.
Amos Makalla leo ameendelea na ziara yake kwa kutembelea Mamlaka ya
Majisafi na Usafi wa Mazingira jijini Tanga (Tanga UWASA) na kujionea
utendaji wa Mamlaka hiyo.
Mhe. Makalla alisikia taarifa ya
utendaji wa Mamlaka hiyo na kufurahishwa nayo, hasa kwa jinsi
walivyofanikiwa kupiga hatua kubwa ya kupunguza kiwango cha upotevu wa
maji kwa kiasi kikubwa na ukusanyaji mzuri wa mapato kutoka kwa wateja
wake.
“Kwa kweli nimefurahishwa mno na
jitihada zenu za kupunguza upotevu wa maji na kwa kufikia kiasi cha
asilimia 23 ni kiwango kizuri, ukilinganisha na Mamlaka nyingine nchini.
Hasa ikizingatiwa hii ni changamoto kubwa na kama Wizara tunafanya
jitahada kupata suluhisho lake,” alisema Makalla.
Pia, aliongeza ukusanyaji mzuri wa
mapato ni hatua kubwa kwa Mamlaka hii, kwani itarahisisha na kuchangia
utendaji mzuri wa kazi na maendeleo ya Mamlaka hiyo katika kuhakikisha
inainua Sekta ya Maji jijini Tanga na mkoa mzima kwa ujumla.
Katika ziara hiyo Mhe. Makalla
amefanikiwa kutembelea miradi ya maji ya vijiji vya Misengeni, Mikwamba
na Michungwani, wilayani Muheza. Na vilevile, chanzo cha maji cha
Mibayani, kituo cha kusukuma na kutibu majisafi cha Mowe na eneo la
ujenzi wa mabwawa ya majitaka lililopo Utofu, Tanga Mjini.
Mhe. Makalla ameanza ziara yake ya
siku 6 jana mkoani Tanga, ikiwa ni hatua ya kuhakikisha utekelezaji wa
programu ya wa Big Results Now na miradi yote ya maji inatekelezwa kwa
kasi na ufanisi ili kuleta matokeo yenye tija na kwa wakati.
Post a Comment