KATIKA
hali inayoashiria kutokukubaliana, mvutano mkali unatarajiwa kuwepo
baina ya baadhi ya waislamu walio wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba na
wale walio nje ya vikao vinavyofanya mchakato wa Katiba mpya.
Mwishoni mwa wiki iliyopita iliyopita, Shura ya Maimamu Tanzania
ilitoa tamko la kupinga rasimu mpya ya Katiba inayopendekezwa baada ya
kubaini kuwa haikuwa na kipengele cha Mahakama ya Kadhi, ambayo walikuwa
wakiipigia upatu ili iwepo.
Katika tamko lao, walisema watafanya kampeni katika misikiti nchi
nzima, wakiwataka wananchi kupiga kura ya hapana. Lakini wakizungumza
bungeni mwanzoni mwa wiki hii, baadhi ya wajumbe wa Bunge hilo walipinga
msimamo wa wenzao, wakidai rasimu hiyo ya katiba ni nzuri.
Mwenyekiti wa Bunge maalum la Katiba Samuel Sitta.
Wakati wajumbe hao wa Bunge maalum wakitoa tamko hilo, mjumbe
mwingine, Sheikh Himid Jongo kutoka kundi la 201, aliungana na Shura ya
Maimamu kwa kusema hatapiga kura kuipitisha rasimu hiyo, kama haitakuwa
na Mahakama ya Kadhi.
Wakati mvutano huo ukiendelea, Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA),
taasisi inayotambuliwa na serikali kama ndiyo chombo rasmi cha waumini
wa dini hiyo kubwa nchini, halijatoa tamko lolote kufuatia kuwasilishwa
kwa rasimu hiyo ya Katiba inayopendekezwa.
- GPL
إرسال تعليق