MWANAFUNZI wa darasa la tatu shule ya Msingi Mnomo, Kata ya
Msangamkuu, Wilaya ya Mtwara Vijijini, Ahmadi Mtuna (10), amefariki
dunia baada ya kujinyonga na kamba ya manila katika kenchi za nyumba
aliyokuwa akiishi.
Tukio hilo, limetokea jana majira ya saa 5 asubuhi, eneo la Kilimani
Kata ya Msangamkuu, ambako Ahmadi wakati akijinyonga familia yake
ilikuwa nyumba ya jirani kwenye Maulidi.
Akizungumza kwa njia ya simu, mama mkubwa wa Ahmadi,
Sikujua Saidi, alisema jana asubuhi walikwenda na Ahmadi kuchoma
korosho maeneo ya barabarani, baada ya kumaliza alimuaga kuwa anarudi
nyumbani ndipo alipomruhusu.
Sikujua, alisema naye baada ya kurudi nyumbani alikuta mlango uko
wazi, ndipo alipoingia ndani kufunga, lakini kabla ya kufanya hivyo
alipotupa jicho juu alimuona Ahmadi ananing’inia, akamuita Ahmadi,
Ahmadi lakini ikawa kimya, ndipo alipotoka nje kukimbia kwenda kuwaita
majirani kwenye Maulidi ili waje wamwangalie na walipofika walikuta
ameshapoteza maisha.
“Inaniuma sana, mwanangu tulikuwa wote muda huu tukichoma korosho
dakika chache tu kaniaga naenda nyumbani, kumbe alikuwa ananiaga
sitaweza kumuona tena hapa duniani… kikweli siamini kabisa na
kilichotokea… Hapa alipojinyongea chini yake tumekuta nazi ambayo
haijatolewa maganda, nadhani alikuwa anacheza baada ya nazi kuteleza
ndipo aliponing’inia na kamba ikamkaba shingoni na umauti ukamkuta,”
alisema Sikujua na kuongeza:
Wakati Ahmadi anajinyonga, Babu na Bibi yake walikwenda nyumba ya
jirani kwenye Maulidi, kwa hiyo nyumbani hakukuwa na mtu, alikuwepo
pekee yake na kamba aliyojinyongea ilikuwa inatumika kufungia mbuzi,
sasa yeye nadhani alikuwa anajaribu kufunga kama anavyofungwa
mbuzi…Tutaongea kila kitu lakini ukweli anao yeye marehemu alichokuwa
anafanya, maana ni mtoto mdogo hana akili ya kujua hiki ninachofanya ni
kitu kibaya, yeye akili yake anajua anacheza kumbe ni hatari.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Augustine Ollomi,
alipotafutwa kwa simu kuthibitisha, alikiri kutokea kwa tukio hilo na
kuwa tayari maofisa wake wamekwishakwenda eneo la tukio na watakaporejea
ofisini na kumpa taarifa, atatoa taarifa zaidi kwa vyombo vya habari.

إرسال تعليق