Aliyekuwa mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba ndugu Haji Ambar Khamis ameangua kilio mbele ya waandishi wa habari na kulazimika kukimbizwa hospitalini kwa matibabu baada ya kukiri chini ya kiapo kuwa hakushiriki na kuipitisha katiba inayopendekezwa licha ya jina lake kuandikwa katika katiba inayopendekezwa aliyokabidhiwa Rais wa jamhjuri ya muungano wa Tanzania huku mwenyekiti wa bunge hilo akitakiwa kuomba radhi kwa kuwalaghai watanzania.
Akitoa tamko la chama cha NCCR Mageuzi juu ya kile alichiokitaja kama kadhia mwenyekiti wa chama hicho mhandisi James Mbatia akizungumza kwa hisia kali katika makao makuu ya chama hicho ameitaka serikali iliyoko madarakani kuwawajibisha wote walioshiriki kubuni na kuandaa kile alichookiita mkakati wa kuhusisha jina la makamu mwenyekiti wa chama hicho taifa-kwa upande wa Zanzibar ndugu Haji Ambar Khamis ambaye jina lake ni namba 39 katika ukurasa wa 209 katika orodha ya majina ya wajumbe wa bunge maalum la katiba walioshiriki na kupitisha katiba inayopendekezwa toleo la Octoba 2014.
Aidha Mh Mbatia ameitaka serikali kutoa tamko la kuwahakikishia usalama wa maisha ya ndugu Haji Ambar Khamis na familia yake samabamba na viongozi wa Ukawa kwa ujumla huku akirejea matukio ya vifo alivyoviita vya kutatanisha vya aliyekuwa mjumbe wa tume ya mabadiliko ya katiba marehemu Dkt Edmund Sengondo Mvungi na aliyekuwa kamishna wa chama hicho mkoa wa Mara hayati Stephen Sebeki na pia kumtaka aliyekuwa mwenyekiti wa bunge hilo kumuomba radhi ndugu Haji na Watanzania kwa ujumla kwa kuwa suala hilo si la bahati mbaya bali ni mkakati uliopangwa.
Akizungumzia kwa hisia kali huku akilengwa lengwa na machozi makamu huyo wa mwenyekiti wa chama hicho kwa upande wa Zanzibar ndugu Haji Ambar Khamis ambaye jina lake limeandikwa katika orodha ya majina ya wajumbe walioshiriki na kupitisha katiba inayopendekezwa amesema kwa namna yeyote ile hakushiriki katika mchakato huo.
Mara baada ya maneno hayo hali ya ndugu Ambar ilibadilika na kushindwa kuendelea na mkutano huo hali iliyolazimu uongozi wa chama hicho kuahirisha baadhi ya shughuli na kumkimbiza hospitalini kwa matibabu zaidi.
Ikumbukwe kuwa azimio la halmashauri kuu taifa ya chama cha NCCR Mageuzi kwa pamoja kiliazimia kutoa adhabu ya kumfukuza uanachama mwanachama yeyote wa NCCR Mageuzi ambaye kwa namna yeyote atashiriki katika vikao vya Bunge maalum la Katiba ambapo sasa jina la makamu mwenyekiti taifa Zanzibar Haji Ambar Khamis linaonekana katika orodha ya majina ya wajumbe wa bunge maalum la katiba walioshiriki na kupitisha katiba inayopendekezwa.
Chanzo: ITV
إرسال تعليق