Phiri afunguka wanaoimaliza Simba

Kocha mkuu wa Simba, Patrick Phiri.
MWENDO wa kusuasua tangu kuanza kwa ligi kuu msimu huu, umeanza kuzua hofu kwa viongozi na wanachama wa kikosi hicho, lakini kocha mkuu, Patrick Phiri ameibuka na kuweka bayana kinachoimaliza timu hiyo.
Phiri ambaye ameshuhudia kikosi chake kikishindwa kuwika mbele ya timu za Coastal Union, Polisi Moro na Stand United kikiwa nyumbani kwenye Uwanja wa Taifa, amefunguka na kutaja ‘mchawi’ mkubwa ni kujiamini kwa wachezaji kabla ya mchezo, msongo wa mawazo pamoja na kuandamwa na majeruhi.
Akizungumzia mwenendo wa kikosi chake, Phiri alisema wachezaji wake wamekuwa na kasumba ya kujiamini kwa kiasi kikubwa, hasa wanapokuwa wakiongoza, ndiyo maana wamekuwa wakianza kwa kasi na kulisakama lango pinzani mara nyingi, lakini hujikuta wakimaliza kwa kuchechemea.
Phiri amekiri kuwa kikosi chake kimekuwa kikicheza vyema dakika 50 hadi 60 huku akitaja sababu kuwa ni kujiamini kwa wachezaji.
“Siyo kusema labda wachezaji wetu wanakosa stamina, hapana, ni hali ya kuridhika na matokeo, hasa timu inapokuwa ikiongoza. Pili, wanakuwa na ‘stress’ kutoka kwa mashabiki hasa pale timu pinzani inaposawazisha, wachezaji hujikuta wakicheza kwa presha, jambo ambalo huwaathiri jumla,” alifunguka Phiri.
Aliongeza kuwa jinamizi la majeruhi kwa kiasi kikubwa limechangia kuharibu programu zake za kusaka kikosi cha kwanza, huku akilia na Paul Kiongera na Ivo Mapunda ambao walitarajiwa kuwa msaada mkubwa Simba.

Post a Comment

Previous Post Next Post