Na Anna Nkinda – Maelezo
Taasisi ya Mwalimu Nyerere kwa
kushirikiana na Makumbusho ya Taifa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa
Tanzania (JWTZ) wameandaa maonyesho na mdahalo wa kukumbuka na kuenzi
mchango wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika
kujenga, kutetea, kulinda na kudumisha amani Duniani.
Maonyesho hayo ya siku tano
ambayo yatafunguliwa tarehe 13 na kumalizika terehe 17 mwezi huu
yatafanyika katika ukumbi wa Makumbusho ya Taifa yaliyopo jijini Dar es
Salaam.
Kwa mujibu wa Taarifa kwa vyombo
vya habari iliyotolewa leo jijini Dar es Salaam na kusainiwa na Gallus
Abedi ambaye ni Msaidizi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu
Nyerere ilisema maonyesho hayo yatajikita zaidi kuonyesha picha,
nyaraka, vitabu, matukio na kazi mbalimbali zinazohusiana na Baba wa
Taifa ambaye ni Rais wa Kwanza na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi
na Usalama ya Tanzania.
Mada zitakazotolewa katika
mdahalo utakaofanyika tarehe 17 ambayo ndiyo siku ya kilele cha
makumbusho hayo ni misingi, utekelezaji na usimamizi wa kujenga, kulinda
na kudumisha amani na uchambuzi na mifano halisi ya Sera za utekelezaji
wa misingi ya kujenga amani kwenye Sekta mbalimbali za maendeleo.
“Top of Form
Bottom of Form
Lengo kuu la maonyesho na mdahalo
huo ni kuwawezesha watanzania na hasa vijana kujifunza na kujua misingi
ambayo Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere aliizingatia katika kujenga,
kutetea, kulinda na kusimamia ili Tanzania iwe nchi ya amani kama ilivyo
leo na pia mchango wake alioutoa kudumisha amani”.
Baadhi ya misingi mikuu
aliyoizingatia ni utu, usawa, haki na heshima kwa binadamu wote. Misingi
hii iliifanya Tanzania iwe kitovu na mbeleko ya harakati za ukombozi wa
Bara la Afrika na utetezi wa haki za wanyonge duniani”, ilisema Taarifa
hiyo.
Aidha watanzania wote na hasa
vijana kutoka vyuo vikuu, Taasisi mbalimbali za elimu na vyuo na shule
za sekondari wameombwa kushiriki katika maonyesho hayo ambayo mgeni
Rasmi atakayefungua ni Mama Kate Kamba ambaye ni Mbunge wa Bunge la
Afrika ya Mashariki.
Maonyesho na mdahalo huo
vimeandaliwa ili viwe sehemu ya maadhimisho ya miaka 15 tangu kifo cha
Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kilipotokea tarehe 14
Oktoba mwaka 1999 katika Hospitali ya Mtakatifu Thomas mjini London
nchini Uingereza. Sherehe za maadhimisho hayo yanafanyika kitaifa mkoani
Tabora.
Post a Comment