Siku moja baada ya Miss Tanzania 2014, Sitti Mtemvu ‘kueleza’
kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii Facebook kulivua taji hilo,
waandaaji wa mashindano hayo, Lino Agency International wamesema
hawajapokea barua rasmi kutoka kwa mrembo huyo ya kulivua taji hilo.
Juzi zilizagaa taarifa kuwa mrembo huyo amelivua
taji baada ya kuwapo ujumbe katika mtandao wa facebook ambao unaonyesha
umeandikwa na mrembo huyo. Ujumbe huo ulisomeka:
“Habari za jioni Watanzania wenzangu, kutokana na
kusemwa maneno mengi yasiyo na tija juu ya hili taji la Umiss Tanzania
mpaka kusababisha nisiwe na amani na uhuru ndani ya nchi yangu, kwa roho
safi nimeamua mwenyewe kulivua taji hilo na kuacha wanayeona anastahili
apewe ili niendelee na maisha yangu kwa amani, isiwe shida sana kwani
sitegemei taji hili ili kuishi.”
Hata hivyo, taarifa ambazo tumezipata
zinasema, Sitti alifikia uamuzi wa kulivua taji baada ya kushauriwa
kufanya hivyo na wizara inayosimamia habari, vijana, utamaduni na
michezo ambayo ilifanya kikao juzi na Mkurugenzi wa mashindano hayo,
Hashimu Lundenga na Katibu Mkuu wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA),
Godfrey Lebejo.
Inaelezwa kuwa kikao hicho kilifanyika kwa ajili
ya kutafuta ukweli kuhusu suala la umri wa Sitti, kwani nyaraka
mbalimbali za mrembo huyo zinaonyesha amezaliwa Mei, 1989 hivyo ana umri
wa miaka 25 wakati moja ya vigezo ambavyo mshiriki wa mashindano ya
Miss Tanzania anatakiwa kuwa navyo ni kuwa na umri usiozidi miaka 24.
Wiki iliyopita Sitti aliingia kwenye kashfa zaidi
ya kudanganya umri baada ya kuibuka na cheti kipya cha kuzaliwa ambacho
kinaonyesha alizaliwa Mei 31, 1991 wakati zipo nyaraka zinaonyesha
alizaliwa mwaka 1989. Nyaraka hizo ni hati yake ya kusafiria na leseni
ya udereva ambayo ilitolewa nchini Marekani.
Chanzo chetu cha habari kinasema, katika kikao
kilichoandaliwa na Wizara ya Habari, Vijana Utamaduni na Michezo
yalifanyika majadiliano ya kina ikiwa ni pamoja na kulinda heshima ya
baba yake Sitti ambaye ni Mbunge wa Temeke, Abbas Mtemvu kwa hiyo mrembo
huyo alishauriwa atangaze mwenyewe kuvua taji hilo.
“Kikao cha Kamati ya Miss Tanzania na familia ya
Mtemvu kitakaa jioni (jana), Sitti mwenyewe ndiye atatakiwa kutangaza
kujivua taji hilo, nadhani baadaye utatolewa
msimamo wa familia ila mpango uliopo ni Sitti aachie taji hilo,”
kilisema chanzo hicho cha habari.

إرسال تعليق