Vyama vya CCM, CUF wavutana kura ya maoni Zanzibar

Na Mwinyi Sadallah, Mwananchi
Ni kuhusu kura ya maoni ya Katiba, CUF wakidai katiba hiyo haikutokana na maoni ya wananchi.
Zanzibar: Wakati Chama cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimesema kitafanya kampeni maalumu kuhakikisha kura ya maoni ya Katiba ya Muungano inashinda Zanzibar, Chama cha Wananchi (CUF) kimesema kinajipanga kufanya kampeni nzito kupinga rasimu hiyo.
Hayo yameelezwa na viongozi wa vyama hivyo hivyo walipozungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti jana, baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Kikwete na Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein, kukabidhiwa Rasimu ya mwisho ya Katiba Oktoba 8, mwaka huu.
Mkurugenzi wa Uenezi na Mawasiliano ya Umma wa CUF, Salim Abdalla Bimani alisema wabunge wa Bunge la Katiba wameshindwa kuheshimu Rasimu iliyotokana na maoni ya wananchi yaliyokusanywa na Tume ya Jaji Joseph Warioba.
Alisema CUF itafanya mikutano ya hadhara katika majimbo yote Unguja na Pemba kuwaelemisha wananchi ubaya wa rasimu hiyo na kama watapitisha Zanzibar itapoteza hadhi yake ya kuwa nchi na Rais wa Zanzibar kukosa mamlaka ya kugawa mipaka ya wilaya na mikoa visiwani humo.
Alisema mambo mengi yaliyotokana na maoni ya wananchi yametupwa na wabunge wa Bunge la Katiba ikiwamo wabunge kuwekewa ukomo, wananchi kuwa na uwezo wa kumuondoa mbunge asiyewajibika, mfumo wa Muungano wa Serikali tatu, kufutwa kwa viti maalumu, pamoja na miiko ya uongozi kutozingatiwa.
Bimani alisema ni vizuri kura ya maoni ikafanyika baada ya uchaguzi mkuu 2015 kama viongozi wa vyama walivyokubaliana na Rais Jakaya Kikwete. Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Vuai ali Vuai alisema Rasimu ya mwisho ya Katiba ni nzuri kwa sababu imegusa makundi mbalimbali wakiwamo watu wenye ulemavu, wavuvi, wakulima , wafugaji pamoja na haki ya kuishi na kuwataka Watanzania kuipokea rasimu hiyo.
Alisema Katiba hiyo siyo ya CCM kama wanavyojaribu kupotosha wapinzani ikizingatiwa vyama 16 vya siasa na makundi maalumu vimeshiriki kikamilifu kujadili na kupitisha rasimu hiyo.
Hata hivyo alisema mambo yaliyorekebishwa katika Rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba na wabunge walizingatia maslahi ya Taifa na wananchi .
Msemaji wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar Idrisa Haji Jecha alisema ZEC inaendelea kuhakiki daftari la wapiga kura wa kudumu ikiwemo kuingiza wapiga kura wapya na kuondoa majina ya watu waliokufa kabla ya kufanyika kwa kura ya maoni Zanzibar.
Hata hivyo alisema mpaka sasa hawajui lini kura ya maoni itafanyika kwavile bado hawajapokea taarifa yoyote kuhusu mchakato huo kutoka Tume ya Taifa ya uchaguzi Tanzania (NEC).
Rasimu ya Katiba inahitaji kuugwa mkono na asilimia 50 ya Wazanzibar na kwa idadi kama hiyo Tanzania bara.
Chanzo Mwananchi

Post a Comment

أحدث أقدم