Picha za mafuvu katika maadhimisho ya miaka 20 ya mauaji ya halaiki nchini Rwanda
Watu walionusurika na mauaji ya halaiki nchini Rwanda wamelaani
makala maalum iliyoandaliwa na kurushwa na kituo cha television cha BBC
II kuhusu mauaji ya Rwanda. Mwandishi wa makala hayo alieleza kwamba
kuanguka kwa ndege ya rais wa zamani nchini Rwanda mwaka 1994 ilikuwa
sababu ya kutokea mauaji ya halaiki nchini humo suala ambalo
linakanushwa vikali na serikali ya Rwanda na walionusurika na mauaji
hayo.
Makala hiyo iliyopewa jina “The untold story about Rwanda” ikiwa na
maana hadithi isiyotajwa kuhusu Rwanda. Mwandishi wake Jane Corbin
ambaye pia ni mwandishi wa habari wa kituo cha televisheni cha BBC
alikwenda Rwanda mwezi April mwaka huu wakati wa kumbukumbu ya mauaji ya
Rwanda ya mwaka 1994. Makala haya yanafafanua jinsi ya mauaji ya Rwanda
yalivyoanza na kufanayika.
Lakini walionusurika na tukio hilo pamoja na serikali kwa jumla
wanaona kile kilichoko kwenye makala hiyo ni upotoshaji wa ukweli
wenyewe na kupinga kabisa kutokea kwa mauaji ya Rwanda.
katika tangazo lililotolewa kwa vyombo vya habari na jumuiya ya
kutetea haki za walionusurika na mauaji hayo IBUKA limelitaka shirika
la habari la BBC kuacha kabisa kutangaza makala hiyo lakini zaidi
kutathmini mienendo ya baadhi ya wafanyakazi wake.
Tangazo hilo linasema kwamba ukweli kwamba mwandishi huyo alikwenda
Rwanda mwaka huu na kushindwa kuzungumza na walionusurika na mauaji hayo
na badala yake akaamua kuzungumza na wapinzania wa serikali ya Rwanda
ambao wengi wao walikuwa na mkono kwenye mauaji hayo ni ishara tosha
kwamba mwandishi huyo Jane Corbin alikuwa na agenda ya siri.
Mwanasheria wa kimataifa ambaye pia ni mmoja wa walionusurika na
mauaji hayo Dr. Bideri Justin anasema sakata hii inaweza kuleta athari.
“Ni uamuzi wa hatari kabisa ambao unapotosha historia ya nchi ya
Rwanda lakini kubwa mauaji ya kimbari ya mwaka 1994. Watu wanaofanya
hivi kwa kiasi kikubwa huwa na maslahi binafsi”.
Katika hatua iliyowakasirisha wengi walionusurika ni pale mwandishi
huyo anapotaja kwamba nchini Rwanda walifariki watu 200,000 tofauti na
idadi inayotajwa na Rwanda ya wahanga milioni moja au ile
iliyoidhinishwa na Umoja wa Mataifa ya watu 800,000.
Vile watu aliowahoji kwenye makala hiyo wengi wao wanatajwa kuwa wapinzani wa serikali ya Rwanda wanaoishi uhamishoni.
Jumuiya inayotetea haki za walionusurika na mauaji hayo inasema
inashangazwa na mwandishi huyo kuamua kuwahoji watu hao na kushindwa
kuwapa nafasi wale walionusurika suala ambalo wanasema ni kukiuka
maadili ya uandishi wa habari ya kutolalia upande wowote.
Hata hivyo mwanasheria Bideri Justin anasema ukweli unabaki pale
pale. “Wengi wanafahamu fika kilichotokea Rwanda, kundi la watu wachache
linalojaribu kupotosha ulimwengu linaweza kuwa hatari lakini ni jukumu
la watu wote kuhakikisha ukweli unabakia bila chembe ya uongo”.
Aidha Makala hiyo inasemaa kwamba kuanguka kwa ndege ya rais wa
zamani wa Rwanda ilikuwa chanzo cha mauaji hayo ya halaiki kitu ambacho
hakipatiwi uzito na serikali pamoja na walionusurika wakisema kwamba
hata kabla ya kutunguliwa ndege hiyo mauaji hayo dhidi ya kabila la
watutsi yalianza zamani.
Haijulikani sakata hii itaishia wapi lakini mwaka 2008 Rwanda iliwahi
kufunga matangazo ya Idhaa ya BBC katika lugha ya kinyarwanda kutokana
na shutuma za kutoa nafasi kwa wapinzani na kutokea kwa mauaji hayo na
kueneza itikadi ya ubaguzi. Lakini baadaye hali ilirudi kuwa ya kawaida.
إرسال تعليق