
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini (CDF), Jenerali Davis Mwamunyange
Tarime. Watu 12 wamejeruhiwa wakati wa mashambulizi ya kurushiana risasi
baina ya askari wa Jeshi la Wananchi (JWTZ) Kikosi 128 KJ cha Nyandoto
na Polisi wa Kituo cha Stendi wilayani Tarime mkoani Mara.
Hatua hiyo imekuja wakati wanajeshi hao walipokuwa wakijaribu kumchukua
askari mwenzao aliyekamatwa na Polisi wa Kikosi cha Usalama Barabarani
kwa kuendesha pikipiki bila kuwa na kofia ngumu.
Mashambulizi hayo ya kurushiana risasi na kutwangana ngumi na mateke yalitokea juzi saa 12 jioni katika Kituo cha Polisi Stendi.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Tarime, Bernard
Makonyo alisema amepokea majeruhi 10, kati ya hao wawili ni askari wa
JWTZ, polisi saba na raia mmoja. Alisema majeruhi tisa wameruhusiwa na
mwingine kupelekwa Hospitali ya Shirati kwa matibabu zaidi.
Dk Makonyo aliwataja waliojeruhiwa kuwa ni Aloyce Filbert (24)
aliyepigwa risasi mguu wa kulia, Deodatus Dominic (26) aliyejeruhiwa
puani na wote ni askari wa JWTZ.
Wengine ni askari polisi saba ambao ni Makoye Katula (26), Sylvester
Michael (31), Salum Omary (44), Abdallah Halifa (24), Joel Msabila (25),
Ally Juma (27) na Deogratius Tryphon (32) na raia Hamza Jumanne (33)
aliyepigwa risasi mguu wa kushoto ambaye alipelekwa Hospitali ya
Shitari, Rorya kwa matibabu.
Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Kipolisi Tarime/Rorya, Ndalama Salumu
anadaiwa kujeruhiwa kwa kupigwa katika vurumai hizo huku mwananchi
mwingine, David Kisaro (20) akijeruhiwa kwa bomu jichoni. Alitibiwa
katika Zahanati ya Tarime.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Tarime/Rorya, Benedict Mambosasa
alisema mwanajeshi aliyekamatwa alifanya makosa kwani baada ya kukamatwa
na kuombwa kwenda kituo cha polisi, alikaidi.
Mambosasa alisema mwanajeshi huyo licha ya kukiuka taratibu, aliwatolea
lugha za matusi polisi jambo lililowalazimu kumkamata kwa nguvu, ndipo
wanajeshi wenzake walipoingilia kati na kusababisha kutokea kwa
majibishano ya risasi za moto. Hata hivyo, alisema hakuna aliyejeruhiwa.
Alisema wanajeshi watatu ambao hawakutajwa majina, wamekamatwa na polisi kwa kuvunja utaratibu wa usalama.
Mkuu wa Wilaya ya Tarime, John Henjewele ambaye pia ni Mwenyekiti wa
Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, amelaani kitendo hicho cha
kurushiana risasi za moto hewani akisema ni cha utovu wa nidhamu na
maadili ya kazi ya jeshi na kwamba hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.
Alisema wananchi Tarime wameshangazwa kwa kitendo kilichofanywa na
walinda usalama hao, wakisema si cha kinidhamu huku wakisema
kilikwamisha shughuli zao kwa muda kwa kuhofia usalama wa maisha yao.
Mkazi wa Tarime, Joseph Samson amesema kitendo hicho kimewashangaza sana wananchi.
MWANANCHI
Post a Comment