*Aridhishwa na ujenzi wa miundombinu, azindua majengo mapya
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema
uamuzi wa Serikali wa kukopa fedha ili kuboresha miundombinu kwenye
taasisi za elimu ya juu nchini ulichukuliwa kwa lengo la kujibu tatizo
la sasa la wingi wa vijana wanaohitimu kidato cha sita.
Ametoa kauli hiyo jana usiku
(Ijumaa, Oktoba 10, 2014) wakati akizungumza na wahadhiri, wakufunzi,
wanafunzi na wanajumuiya ya Chuo Kikuu Huria (OUT) mara baada ya
kuzindua jengo la ghorofa 10 linalojulikana kama Ghorofa la Elimu ya
Masafa ya Huria (Open Distance Learning Tower – ODL Tower) lililogharimu
sh. bilioni 3.
Waziri Mkuu ambaye aliwasili
jijini Dar es Salaam jana mchana akitokea Morogoro, alitembelea Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam pamoja na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania ili
kukagua utekelezaji wa mradi wa Sayansi na Teknolojia ya Elimu ya Juu
(Science and Technology Higher Education Project – STHEP) unaoendeshwa
chini ya uhisani wa Benki ya Dunia.
“Mradi huu ni wa miaka mitano
ambao ulianza mwaka 2009 na unakamilika mwaka huu. Lengo hasa lilikuwa
ni kujenga uwezo wa wataalamu wetu ambao watakuja kufundisha watoto wa
kidato cha sita ambao idadi yao inazidi kuongezeka kila mwaka.”
Alisema Serikali iliridhia pia
fedha hizo zitumike kujenga miundombinu mipya ya kufundishia pamoja na
kukarabati baadhi ya zamani kwani kama miundombinu haipo, kazi ya
kufundisha haitakuwepo.
“Tulikubaliana pia fedha hizo
zinunue vifaa kwa maana ya kompyuta, vifaa vya maabara pamoja na samani
za maktaba na baadhi ya madarasa. Ni fedha za mkopo lakini zimetumika
kusaidia Watanzania wote.”
Chini ya uhisani wa mradi huo,
Chuo Kikuu Huria kimesomesha wahadhiri 29 kati 12 ni masomo ya Uzamifu
na 17 ni masomo ya uzamili. Pia kimejenga Maabara za kompyuta tatu,
maktaba ya kuweka watu 224 kwa wakati mmoja, vyumba vya mihadhara
(seminar rooms) maabara ya lugha (language lab), ununuzi wa kompyuta na
samani.
Mapema akiwa katika Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam, Waziri Mkuu alikagua majengo mapya ya ghorofa la shule
kuu ya elimu, sayansi ya majini (Aquatic Sciences and Technologies),
Multi Complex Building ambalo litakuwa na kituo cha wanafunzi, pamoja
kuzindua jengo jipya la Uhandisi Migodi na Usindikaji Madini (Mining and
Mineral Processing Building) lililopo kwenye Chuo cha Uhandisi na
Teknolojia (College of Engineering Technology).
Akitoa taarifa ya miradi yote
hiyo, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof. Rwekaza
Mukandala alisema katika awamu hii ya kwanza ya mradi wa STHEP, Chuo
hicho kilifanikiwa kupata ufadhili wa Dola za Marekani milioni 40.79
(sawa na sh. bilioni 67).
Chini ya mradi huo, Prof.
Mukandala alisema chuo kimefanikiwa kuendeleza kimasomo wafanyakazi wake
zaidi ya 150, kujenga majengo mapya manane, kusomesha wahadhiri
tarajiwa 163 ambapo 63 wamesoma shahada za umahiri (masters) na
67wamepata shahada za uzamivu (Ph.D).
“Tumeweza kununua vifaa mbalimbali
vikiwemo vya maabara, kompyuta 864, vitabu zaidi ya 960, na vifaa vya
teknolojia, uhandisi na sayansi. Pia tumeweza kupanua madarasa, maabara
na ofisi .”
“Tumepata maabara mpya 49
zitakazokuwa zikitumiwa na wanafunzi 3,630 kwa wakati mmoja; madarasa 53
yenye uwezo wa kubeba wanafunzi 4,200 kwa wakati mmoja; ofisi 322
zitakatumiwa na wafanyakazi wasiopungua 600,” aliongeza.
Post a Comment