WAZIRI MKUU AKAGUA CHUO KIKUU DAR NA CHUO KIKUU HURIA


 *Aridhishwa na ujenzi wa miundombinu, azindua majengo mapya
 WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema uamuzi wa Serikali wa kukopa fedha ili kuboresha miundombinu kwenye taasisi za elimu ya juu nchini ulichukuliwa kwa lengo la kujibu tatizo la sasa la wingi wa vijana wanaohitimu kidato cha sita.
Ametoa kauli hiyo jana usiku (Ijumaa, Oktoba 10, 2014) wakati akizungumza na wahadhiri, wakufunzi, wanafunzi na wanajumuiya ya Chuo Kikuu Huria (OUT) mara baada ya kuzindua jengo la ghorofa 10 linalojulikana kama Ghorofa la Elimu ya Masafa ya Huria (Open Distance Learning Tower – ODL Tower) lililogharimu sh. bilioni 3.
Waziri Mkuu ambaye aliwasili jijini Dar es Salaam jana mchana akitokea Morogoro, alitembelea Chuo Kikuu cha Dar es Salaam pamoja na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania ili kukagua utekelezaji wa mradi wa Sayansi na Teknolojia ya Elimu ya Juu (Science and Technology Higher Education Project – STHEP) unaoendeshwa chini ya uhisani wa Benki ya Dunia.
“Mradi huu ni wa miaka mitano ambao ulianza mwaka 2009 na unakamilika mwaka huu. Lengo hasa lilikuwa ni kujenga uwezo wa wataalamu wetu ambao watakuja kufundisha watoto wa kidato cha sita ambao idadi yao inazidi kuongezeka kila mwaka.” 
Alisema Serikali iliridhia pia fedha hizo zitumike kujenga miundombinu mipya ya kufundishia pamoja na kukarabati baadhi ya zamani kwani kama miundombinu haipo, kazi ya kufundisha haitakuwepo. 
“Tulikubaliana pia fedha hizo zinunue vifaa kwa maana ya kompyuta, vifaa vya maabara pamoja na samani za maktaba na baadhi ya madarasa. Ni fedha za mkopo lakini zimetumika kusaidia Watanzania wote.” 
Chini ya uhisani wa mradi huo, Chuo Kikuu Huria kimesomesha wahadhiri 29 kati 12 ni masomo ya Uzamifu na 17 ni masomo ya uzamili. Pia kimejenga Maabara za kompyuta tatu, maktaba ya kuweka watu 224 kwa wakati mmoja, vyumba vya mihadhara (seminar rooms) maabara ya lugha (language lab), ununuzi wa kompyuta na samani. 
Mapema akiwa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Waziri Mkuu alikagua majengo mapya ya ghorofa la shule kuu ya elimu, sayansi ya majini (Aquatic Sciences and Technologies), Multi Complex Building ambalo litakuwa na kituo cha wanafunzi, pamoja kuzindua jengo jipya la Uhandisi Migodi na Usindikaji Madini (Mining and Mineral Processing Building) lililopo kwenye Chuo cha Uhandisi na Teknolojia (College of Engineering Technology).
Akitoa taarifa ya miradi yote hiyo, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof. Rwekaza Mukandala alisema katika awamu hii ya kwanza ya mradi wa STHEP, Chuo hicho kilifanikiwa kupata ufadhili wa Dola za Marekani milioni 40.79 (sawa na sh. bilioni 67).
Chini ya mradi huo, Prof. Mukandala alisema chuo kimefanikiwa kuendeleza kimasomo wafanyakazi wake zaidi ya 150, kujenga majengo mapya manane, kusomesha wahadhiri tarajiwa 163 ambapo 63 wamesoma shahada za umahiri (masters) na 67wamepata shahada za uzamivu (Ph.D). 
“Tumeweza kununua vifaa mbalimbali vikiwemo vya maabara, kompyuta 864, vitabu zaidi ya 960, na vifaa vya teknolojia, uhandisi na sayansi. Pia tumeweza kupanua madarasa, maabara na ofisi .”
“Tumepata maabara mpya 49 zitakazokuwa zikitumiwa na wanafunzi 3,630 kwa wakati mmoja; madarasa 53 yenye uwezo wa kubeba wanafunzi 4,200 kwa wakati mmoja; ofisi 322 zitakatumiwa na wafanyakazi wasiopungua 600,” aliongeza.

Post a Comment

أحدث أقدم