Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai(DCI), Isaya Mungulu amesema jalada la upelelezi wa kesi ya mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe limeshakabidhiwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) kwa ajili ya kumfikisha mahakamani. DCI Mungulu alisema hayo jana alipozungumzia mwafaka wa shauri la mwenyekiti huyo aliyetangaza maandamano ya amani kwa wafuasi wa chama chake mara baada ya kuchaguliwa tena kukiongoza kwa miaka mitano mingine.
Alisema DPP ndiye mwenye uamuzi wa lini Mbowe atafikishwa mahakamani baada ya uchunguzi kukamilika.
“Sisi tulishakamilisha taratibu zinazotuhusu na tayari tumeshapeleka jalada kwa DPP. Yeye ndiye mwenye mamlaka ya kuamua lini kesi hiyo itafikishwa mahakamani,” alisema.
Mbowe alitangaza maandamano hayo ya amani nchi nzima mara tu alipochaguliwa kuiongoza Chadema kwa msimu wa tatu, mapema Septemba mwaka huu katika siku aliyotimiza miaka 53 ya kuzaliwa kwake.
Baada ya kutoa tamko hilo, Jeshi la Polisi lilimwita kumhoji kwa zaidi ya saa nne kwa madai kuwa kauli yake ilikuwa na mlengo wa kichochezi.
Aidha, polisi walilazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya wafuasi waliomsindikiza mwenyekiti huyo makao makuu ya jeshi hilo.
Kutokana na tamko hilo la mwenyekiti, wafuasi wa chama hicho waliendesha maandamano katika mikoa mbalimbali na kuwapa polisi wakati mgumu kuyadhibiti kutokana na kutoyatambua kisheria.
Kuhusu utekelezaji wa tamko la mwenyekiti huyo, Mngulu alisema kuwa jeshi lake linaendelea na taratibu za kuwafikisha mahakamani makada wote waliokataa kutii amri halali iliyotolewa kuwaonya kuhusu maandamano hayo.
“Licha ya kwamba tulitoa angalizo hilo, lakini wengi walikaidi amri yetu, japokuwa tulijitahidi na kuyazima. Wapo watu kadhaa tunawashikilia katika mikoa ya Mwanza, Dar es Salaam, Mtwara, Dodoma na Mara. Hatua za kisheria zinaendelea kuchukuliwa dhidi yao,” alisema.
إرسال تعليق