WAZIRI MKUU AKAGUA TIMU ZA VIONGOZI WA DINI

 *Ataka Watanzania wajitokeze kwa wingi Oktoba 12

WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amewataka Watanzania wajitokeze kwa wingi kushangilia mechi ya viongozi wa dini wa mkoa wa Dar es Salaam itakayochezwa Jumapili, Oktoba 12, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Ametoa kauli hiyo leo asubuhi (Ijumaa, Oktoba 10, 2014) wakati akizungumza na wachezaji wa timu za AMANI na MSHIKAMANO zinazoundwa na Masheikh, Maaskofu, Maimamu na Wachungaji kutoka madhehebu mbalimbali ya mkoa wa Dar es Salaam ambao wamepiga kambi mjini Morogoro.

“Hii haijapata kutokea… katika hali ya kawaida mkusanyiko kama huu siyo rahisi na katika nchi nyingine kupata mjumuiko kama huu haiwezekani,” alisema wakati akiongea nao kwenye viwanja vya michezo vya taasisi ya Highlands Baptist Mission iliyoko Kigurunyembe, Morogoro.

Alisema uamuzi wa viongozi wa dini kukaa pamoja na kucheza mechi hiyo ni kutaka kuonyesha dhamira ya kweli ya kufanya mshikamano na amani kuwa ajenda ya kudumu kwa Taifa hili.

“Mimi ninaamini kinachotuunganisha siyo dini bali ni kutambua kwamba sisi sote tumeumbwa na Mungu… sisi sote ni bin-adam. Dini ni milango tu ya kutusaidia tufike kule ambako Mwenyezi Mungu anataka tuende,” alisema.

“Ukichukulia mfano wa wakristo, kuna madhehebu mengi. Kwa hiyo hawa wakigombana tayari ni tatizo. Hivyo uamuzi wa kuwachanganya katika timu ni jambo zuri, ni kudumisha umoja, amani na mshikamano,” aliongeza.

“Hii ni hatua ya kwanza kinachofuata sasa ni kuwa na One Destiny, One People, One Nation,” akimaanisha kuwa na Lengo Moja, Watu Wamoja na Taifa Moja. Alisema hiyo ni kama sura ya kwanza imefunguliwa hivyo, hawana budi kuendelea mbele.

Mapema, Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Alhad Mussa Saleem alimweleza Waziri Mkuu kwamba timu hizo ziko kambini hapo tangu Jumatano, Mei 8, 2014. Alisema leo baada ya mazoezi watakwenda kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Mikumi na kurejea kambini Morogoro. Wanatarajia kurejea jijini Dar es Salaam kesho (Jumamosi) tayari kwa pambano lao la Jumapili, Oktoba 12, 2014.

Waziri Mkuu ambaye aliwasili Morogoro jana mchana akitokea Dodoma, alifanya ziara ya siku kwa kutembelea Chuo Kikuu cha Sokoine na leo atatembelea Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Chuo Kikuu Huria kukagua miradi kama hiyo.

 (mwisho)

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
11410 – DAR ES SALAAM.
IJUMAA, OKTOBA 10, 2014

Post a Comment

أحدث أقدم