Sintofahamu hiyo ilianza baada ya Mbunge wa
Kishapu (CCM), Suleiman Nchambi kuanza kuzungumzia amri iliyotolewa na
Mahakama kuhusu Bunge kujadili ripoti ya IPTL.
Kelele, zomea zomea na kauli za “umechukua hela
wewe” zilisikika kupitia vipaza sauti vya wabunge hao hata kabla ya
mbunge huyo kujenga hoja yake.
Nchambi hakujali kelele hizo na aliwaambia waliokuwa wakizomea... “mkimaliza kuzomea nitaendelea.”
Kutokana na kelele hizo, Zungu alisimama na
kuwaomba wabunge kutulia na kuvumiliana akisema kila atakayesimama
kuomba mwongozo atapewa nafasi.
“Waheshimiwa wabunge oda please! Waheshimiwa
wabunge Bunge linaendeshwa kwa kanuni na kila atakayesimama leo (jana)
na kuomba mwongozo kiti kitampa nafasi, mwacheni aombe mwongozo wake
(wabunge wakaendelea kupiga kelele). Natoa onyo la mwisho kama
hamtasikiliza nitasitisha Bunge sasa hivi na mtabaki mnasema miongozo
yenu canteen (kwenye mgahawa),” alisema Zungu.
Baada ya kauli ya Zungu, wabunge walitulia na
Nchambi akaendelea na kusema wakili ambaye amepeleka kesi hiyo
mahakamani ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema. Alisema wakati wabunge wa
CCM wanataka suala hilo lijadiliwe ili Watanzania wajue nini
kinaendelea, mwanasheria huyo wa Chadema amekwenda kulipinga mahakamani
hivyo akaomba mwongozo wa kiti cha kwa nini suala hilo limefikia hapo na
kwamba kwa nini wakili huyo asijadiliwe.
Kutokana na madai hayo, Mbunge wa Iramba Mashariki
na Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu alisimama na kufafanua kuwa
wakili wa IPTL na PAP ni Gabriel Mnyele wa Mpanda na kwamba ni kweli
mjumbe wa Kamati Mkuu wa Chadema, Mabere Marando anafanya kazi katika
kampuni aliyomo wakili huyo lakini hakuhusika kufungua kesi hiyo.
Baada ya ufafanuzi huo, Lissu aliongeza kuwa
kilichotokea juzi kwa Mahakama kuzuia mjadala bungeni hakijawahi kutokea
tangu Mahakama ya Tanganyika ianzishwe mwaka 1922 na kuwa kinakiuka
Ibara ya 100 ya Katiba ya nchi, hivyo mjadala uendelee.
Aliyefuata alikuwa Mbunge wa Simanjiro (CCM),
Christopher Ole Sendeka ambaye aliomba mwongozo akieleza kuwa Ibara ya
100 ya Katiba inalipa Bunge uhuru wa kujadili suala hilo kwa kuwa macho
ya Watanzania wote yapo Dodoma na wanasubiri Bunge liungane bila mpasuko
wa itikadi za kisiasa... “Wanasubiri kusikia na kupata vielelezo vya
Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) ili waweze kujua nini kinaendelea.”
Mbunge wa Gando (CUF), Khalifa Suleiman Khalifa
aliomba mwongozo akieleza kushangaa kwa nini wabunge walikuwa na haraka
na jambo hilo wakati Spika, Anne Makinda alishatoa mwongozo wa suala
hilo.
“Spika alichosema jana (juzi) ndiyo ruling
(uamuzi) ya Bunge kwa sababu hata mtu aende msikitini au kanisani
itakuja tu,” alisema Khalifa.
- Mwananchi.
- Mwananchi.
إرسال تعليق