
MBUNGE wa Same Mashariki, Anne Kilango (CCM), ameilipua Serikali
kuwa kutokana na kuwa legelege ndio maana nchi za nje zimeifanya
Tanzania kuwa sehemu ya kuuzia dawa za kulevya.
Kilango alitoa kauli hiyo jana bungeni wakati akiuliza swali la
nyongeza kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera na Uratibu wa
Bunge, William Lukuvi.
Alisema kuwa baadhi ya nchi za nje yakiwemo mataifa ya Nigeria na
Pakistan, yameiona Tanzania ndio nchi ya kuuzia dawa hizo za kulenya
kutokana na kuwa legelege, jambo ambalo ni hatari.
Pia, Mbunge huyo aliihoji Serikali kwanini isiendeshe kesi
zinazohusiana na dawa za kulevya kwa siku 14 ili kuondoa mianya ya
rushwa.
Aidha, Kilango aliitaka Serikali iweke wazi suala la uteketezaji wa
dawa hizo za kulevya kwa wananchi ili nao waweze kujiridhisha kuhusiana
na uteketezwaji huo.
Akijibu swali hilo, Lukuvi alisema kuwa sheria ya kupambana na dawa
za kulevya ina mapungufu makubwa sana hata ikilinganishwa na nchi ya
Bangladesh, kwani Wakili wa nchi hiyo hukaa uwanja wa ndege na mtu
anapobainika kukutwa na dawa hizo, husomewa kesi yake hapo hapo.
“Sheria yetu ina mapungufu makubwa na kutokana na mapungufu haya,
hivi sasa tupo katika utaratibu wa kuleta Muswada wa Sheria ya
kupambana na dawa za kulevya ili kuweza kukabiliana na tatizo hili,
kwani hapa nchini hata mtu ukimkamata na dawa hadi zipelekwe kwa Mkemia
Mkuu wa Serikali,” alisema.
Katika swali la msingi, Mbunge huyo alitaka kujua mara dawa za kulevya zinapokamatwa huwa zinapelekwa wapi?
Akijibu swali hilo, Lukuvi alisema kuwa dawa za kulevya zilizokamatwa
huhifadhiwa na kutumika mahakamani kama vielelezo katika uendeshaji wa
kesi husika.
“Baada ya kesi kukamilika, dawa hizo huharibiwa au kuteketezwa kwa
amri ya mahakama kama ilivyoelekezwa katika kifungu cha 34 cha Sheria
ya kupambana na biashara haramu ya dawa za kulevya sura ya 95,”
alisema.
Lukuvi, alisema uteketezaji wa dawa hizo za kulevya umewahi kufanyika
mwaka 2012, ambako kilo 92.2 za Heroin zilitekelezwa katika Kiwanda
cha Saruji Tanga kwa amri ya mahakama, ambako mwaka 2013 kilo 412.7 za
bangi ziliteketezwa, kilo 12.3 za Heroin na kilo 5.6 za Cocaine
ziliteketezwa katika kiwanda cha Saruji Wazo Hill jijini Dar es Salaam
إرسال تعليق