Dodoma. Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Kidawa Hamid Saleh amesema
majengo ya ofisi nyingi za balozi za Tanzania nje ya nchi, zinahitaji
ukarabati au kujengwa upya kwa sababu yaliyopo sasa ni mabovu na ni
hatari kwa maisha ya watu.
“Serikali ina mkakati gani mahususi wa ujenzi wa
majengo hayo ili kuepuka hatari inayoweza kutokea, pamoja na aibu
tunayoipata kama Watanzania na Taifa kwa ujumla?” alihoji Kidawa.
Akijibu swali hilo bungeni jana, Naibu Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mahadhi Juma Maalim alisema
kwa muda mrefu hakukuwa na fedha za bajeti ya maendeleo kwa ajili ya
ununuzi, ujenzi na ukarabati wa majengo ya Serikali yaliyopo balozini.
“Kuanzia kipindi cha mwaka 1961 hadi 1987 ununuzi,
ujenzi na ukarabati wa majengo ulitekelezwa kwa kutumia fedha za
matumizi mengineyo, ambazo kimsingi hazikuweza kukidhi mahitaji kutokana
na ufinyu wa bajeti,” alisema.
Alisema kwa kutambua umuhimu wa ununuzi, ujenzi na
ukarabati wa majengo ya ofisi na makazi, kuanzia mwaka wa fedha
2007/2008, Serikali ilianza kuipatia wizara yake mgawo wa bajeti ya
maendeleo.
“Mkakati mahususi wa wizara ni kuendelea kutumia
fedha za bajeti ya maendeleo zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya
kutekeleza miradi iliyopo balozini,” alisema.
“Hivi sasa wizara ipo katika hatua nzuri ya
majadiliano na NSSF (Mfuko wa Hifadhi ya Jamii ya Taifa),
yatakayowezesha kutekeleza mradi ujenzi wa majengo ya ofisi na kitega
uchumi Nairobi, Kenya,” alisema.
Post a Comment