Watanzania wengi wanamiliki hisa

Dar es Salaam. Utafiti mpya wa kampuni 100 bora zenye ukubwa wa kati umebaini kuwa asilimia 73 ya wafanyakazi wake ni Watanzania wanaomiliki asilimia 55 ya hisa zote.
Akitoa matokeo ya utafiti huo jana, Mkurugenzi Mtendaji wa Research Solutions Africa, Dk Jasper Grosskurth alisema asilimia 45 ya hisa kwenye kampuni nchini zinamilikiwa na watu kutoka nje ya nchi.
Dk Grosskurth alisema kampuni zilizofanikiwa kuingia katika 100 bora mwaka huu zinatarajiwa kutajwa leo katika Ukumbi wa Mlimani City.
Alisema hali ya uchumi kwa kampuni nyingi ilikuwa mbaya mwaka jana ikilinganishwa na 2012.
Hata hivyo, Dk Grosskurth alisema asilimia 78 ya kampuni zilizofanikiwa kuingia kwenye nafasi hiyo zipo Dar es Salaam, kati ya hizo asilimia 38 hazina matawi mikoani.
Pia alisema kati ya kampuni hizo, tatu pekee ndiyo zinazouza bidhaa barani Asia, jambo linalosababishwa na wafanyabiashara kuweka nguvu zaidi katika soko la ndani.
“Asilimia 50 ya kampuni zina mpango wa kufungua matawi nje ya nchi na kila kampuni ina mpango wa kuongeza idadi ya wafanyakazi,” alisema.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mwananchi Communications Ltd, Francis Nanai, ambao ni wadhamini, alisema lengo la utafiti huo unaofanyika kila mwaka ni kuangalia na kuzitambua kampuni zinazokua.
“Leo (jana) tulikuwa nao washiriki ili kuwashirikisha mbinu mbalimbali za kukuza biashara…kesho (leo) washindi watatambuliwa rasmi,” alisema Nanai.
Pia aliwashauri wafanyabiashara kuendelea kushiriki kwenye tafiti hizo kila mwaka kwa kuwa ndiyo njia ya kupima utendaji wa biashara zao.
Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Travel Partner, Erick Mashauri alisema uvumilivu na ujasiri ndiyo njia pekee ya kufikia mafanikio katika biashara.
- Mwananchi

Post a Comment

Previous Post Next Post