Unaingia katika wodi ya wazazi katika hospitali ya wilaya,
unaziona sura za wanawake walio katika uchungu wa kujifungua zikiwa
shakani.Kwanza ni uchungu wenyewe na pili wasiwasi mkubwa iwapo
watakiepuka kifo wakati wa tendo hilo la kuleta uhai duniani.
Aghalabu, wanawake wanaopata ujauzito katika Tanzania huambiwa: “Sali sana, kuzaa mguu mmoja jehanamu mmoja duniani.”
Wauguzi, wakunga na madaktari nao wanajua kuwa kujifungua katika wodi hizi ni kufa au kupona lakini wanaendelea kuwajibika.
Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaweka
wazi kuwa asilimia 99 ya vifo vya uzazi vinatokea katika nchi za Afrika
na nusu ya vifo hutokea katika nchi zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Katika ufafanuzi huo wa takwimu za WHO inaeleza
zaidi kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi 10 duniani zinazoongoza kwa
kukumbwa na vifo vya uzazi.
Hapa nchini, wanawake 21 hadi 24 hufariki kila siku kwa sababu za uzazi.
Hivyo katika kila saa moja, watoto 144 hufariki dunia.
Mratibu wa Taifa wa Muungano wa Utepe Mweupe wa
Uzazi Salama Tanzania, Rose Mlay anasema tatizo la vifo vya uzazi
halijapewa kipaumbele kama ambavyo mambo mengine yanapewa uzito hapa
nchini na kutatuliwa.
Anafafanua zaidi na kusema kuwa kama changamoto za
uzazi katika hospitali zetu zingetatuliwa, basi tungekuwa na Taifa
imara na lenye watoto wenye afya.
“Natafakari ingekuwa vipi iwapo suala la vifo vya
uzazi lingepewa umuhimu kama yanavyopewa matukio mengine kama saratani,
Ukimwi na majanga mengine,” anasema
Anaelezea ukubwa wa tatizo la uzazi na kusema
linatazamwa kama tukio la kawaida wakati ni janga kwani linamaliza
maisha ya wanawake ambao ndiyo wazalishaji wenyewe na kizazi ambacho
kingekuwa taifa la kesho.
“Nadhani tunalichukulia kimazoea kwa sababu vifo
vya uzazi vilianza kuongezeka na kuonyesha hali ya hatari tangu mwaka
1999, wanawake wengi mno wanapoteza maisha,” anasema Mlay.
- Mwananchi
- Mwananchi
Post a Comment