Dar es Salaam. Utafiti mpya wa kampuni 100 bora zenye ukubwa wa
kati umebaini kuwa asilimia 73 ya wafanyakazi wake ni Watanzania
wanaomiliki asilimia 55 ya hisa zote.
Akitoa matokeo ya utafiti huo jana, Mkurugenzi
Mtendaji wa Research Solutions Africa, Dk Jasper Grosskurth alisema
asilimia 45 ya hisa kwenye kampuni nchini zinamilikiwa na watu kutoka
nje ya nchi.
Dk Grosskurth alisema kampuni zilizofanikiwa
kuingia katika 100 bora mwaka huu zinatarajiwa kutajwa leo katika Ukumbi
wa Mlimani City.
Alisema hali ya uchumi kwa kampuni nyingi ilikuwa mbaya mwaka jana ikilinganishwa na 2012.
Hata hivyo, Dk Grosskurth alisema asilimia 78 ya
kampuni zilizofanikiwa kuingia kwenye nafasi hiyo zipo Dar es Salaam,
kati ya hizo asilimia 38 hazina matawi mikoani.
Pia alisema kati ya kampuni hizo, tatu pekee ndiyo
zinazouza bidhaa barani Asia, jambo linalosababishwa na wafanyabiashara
kuweka nguvu zaidi katika soko la ndani.
“Asilimia 50 ya kampuni zina mpango wa kufungua
matawi nje ya nchi na kila kampuni ina mpango wa kuongeza idadi ya
wafanyakazi,” alisema.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mwananchi Communications
Ltd, Francis Nanai, ambao ni wadhamini, alisema lengo la utafiti huo
unaofanyika kila mwaka ni kuangalia na kuzitambua kampuni zinazokua.
“Leo (jana) tulikuwa nao washiriki ili
kuwashirikisha mbinu mbalimbali za kukuza biashara…kesho (leo) washindi
watatambuliwa rasmi,” alisema Nanai.
Pia aliwashauri wafanyabiashara kuendelea
kushiriki kwenye tafiti hizo kila mwaka kwa kuwa ndiyo njia ya kupima
utendaji wa biashara zao.
Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Travel
Partner, Erick Mashauri alisema uvumilivu na ujasiri ndiyo njia pekee ya
kufikia mafanikio katika biashara.
- Mwananchi
- Mwananchi
إرسال تعليق