Wanamgambo wa kitakfiri wa kundi la Boko Haram wa huko Nigeria wamewauwa
wachuuzi wa samaki wasiopungua 48 huko katika jimbo la Borno kaskazini
mashariki mwa nchi hiyo.
Hayo yemeripotiwa na Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Samaki ya Nigeria.
Abubakar Gamandi, Mkuu wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Samaki ya
Nigeria amesema leo kuwa wahanga wa mauaji hayo waliuawa baada ya
wanamgambo wa Boko Haram kuweka kizuizi barabarani katika eneo la Dagon
Fili na kusimamisha msafara wao Alkhamisi iliyopita.
Kwa mujibu wa Gamandi, makumi ya wanamgambo wa Boko Haram siku ya
Alkhamisi walizuia njia inayounganisha Nigeria na Chad karibu na kijiji
cha uvuvi cha Doron Baga katika ufukwe wa Ziwa Chad na kuuwa kundi la
wachuuzi wa samaki 48 waliokuwa wakielekea Chad kununua samaki.
Mkuu wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Samaki ya Nigeria amesema kuwa
wanamgambo wa Boko Haram waliwauwa wachuuzi kadhaa wa samaki na kuwatupa
wengine ziwani ili wazame baada ya kuwafunga mikono na miguu yao ili
wasiweze kuogelea.
Chanzo: kiswahili.irib.ir
إرسال تعليق