Miongoni mwa shule ambazo zimefanya vizuri kitaifa, ni Shule ya
Msingi ya Alliance iliyoko Wilaya ya Nyamagana, jijini Mwanza. Imeshika
nafasi ya nne katika mtihani wa kuhitimu darasa la saba, mwaka huu.
Pamoja na kutumia walimu wa kigeni, mkurugenzi
mtendaji wa Alliance, James Bwire anasema kitaaluma walimu wa Kitanzania
wana uwezo mkubwa na hawawezi kulinganishwa na Wakenya na Waganda.
“Wala mtu asikudanganye kuwa Wakenya wana uwezo
mkubwa kuliko Watanzania. Nimekaa nao, nimeangalia, nimekaa na Waganda,
Wakenya na Watanzania lakini Watanzania wana uwezo mkubwa sana. Ukimkuta
Mtanzania ana uwezo ni wa kweli wala siyo wa kubahatisha,” anasema.
Anasema wanalazimika kuwatumia walimu kutoka nchi
jirani kwa kuwa ni vigumu kupata walimu mahiri wazawa, kwani
wanapomaliza masomo, Serikali inawapangia kazi katika shule za umma.
“Kwa mfano, somo la Maarifa ya Jamii unakuta
tunatumia Wakenya kwa sababu Watanzania hatuwapati, lakini ufundishaji
wa Wakenya si mzuri ndiyo maana ufanisi unashuka hata hesabu tunawatumia
haohao,” anasema.
“Natamani sana kuona walimu wawe wengi na sisi
tuweze kuajiri tufaidi matunda ya Watanzania wenzetu, lakini
hawapatikani. Kupata walimu wazalendo wenye uwezo ni shida kwa kuwa
wanaajiriwa na Serikali moja kwa moja wanapotoka vyuoni.”
Anasema katika kipindi hiki ambacho jitihada za
kuongeza vyuo vya ualimu zinapamba moto, Serikali iangalie umuhimu wa
kuzipatia shule za binafsi walimu wazalendo.
Tuhuma za rushwa kwa shule bora
Mara kwa mara shule binafsi zinazofanya vizuri
zimekuwa zikishutumiwa kutumia rushwa ili kukuza ufaulu lengo likiwa ni
kuzipaisha kwa ajili ya kuvutia soko.
Kama mdau wa elimu, Bwire anasema tuhuma za rushwa
ni uvumi tu lakini ukweli ni kuwa shule nyingi za binafsi zilizo makini
zinafanya vizuri kutokana na kuwekeza katika mikakati na juhudi.
“Kwa mfano, tuchukulie shule yetu ya Alliance kwa
taratibu zetu tulizojiandalia, mwanafunzi akifika darasa la sita lazima
akae bweni, lazima saa 11:00 jioni ahudhurie vipindi na akae mpaka saa
3:30 usiku kila siku,” anasema.
Post a Comment