Bwire: Walimu wa Kitanzania wana uwezo kuliko wageni

Miongoni mwa shule ambazo zimefanya vizuri kitaifa, ni Shule ya Msingi ya Alliance iliyoko Wilaya ya Nyamagana, jijini Mwanza. Imeshika nafasi ya nne katika mtihani wa kuhitimu darasa la saba, mwaka huu.
Pamoja na kutumia walimu wa kigeni, mkurugenzi mtendaji wa Alliance, James Bwire anasema kitaaluma walimu wa Kitanzania wana uwezo mkubwa na hawawezi kulinganishwa na Wakenya na Waganda.
“Wala mtu asikudanganye kuwa Wakenya wana uwezo mkubwa kuliko Watanzania. Nimekaa nao, nimeangalia, nimekaa na Waganda, Wakenya na Watanzania lakini Watanzania wana uwezo mkubwa sana. Ukimkuta Mtanzania ana uwezo ni wa kweli wala siyo wa kubahatisha,” anasema.
Anasema wanalazimika kuwatumia walimu kutoka nchi jirani kwa kuwa ni vigumu kupata walimu mahiri wazawa, kwani wanapomaliza masomo, Serikali inawapangia kazi katika shule za umma.
“Kwa mfano, somo la Maarifa ya Jamii unakuta tunatumia Wakenya kwa sababu Watanzania hatuwapati, lakini ufundishaji wa Wakenya si mzuri ndiyo maana ufanisi unashuka hata hesabu tunawatumia haohao,” anasema.
“Natamani sana kuona walimu wawe wengi na sisi tuweze kuajiri tufaidi matunda ya Watanzania wenzetu, lakini hawapatikani. Kupata walimu wazalendo wenye uwezo ni shida kwa kuwa wanaajiriwa na Serikali moja kwa moja wanapotoka vyuoni.”
Anasema katika kipindi hiki ambacho jitihada za kuongeza vyuo vya ualimu zinapamba moto, Serikali iangalie umuhimu wa kuzipatia shule za binafsi walimu wazalendo.
Tuhuma za rushwa kwa shule bora
Mara kwa mara shule binafsi zinazofanya vizuri zimekuwa zikishutumiwa kutumia rushwa ili kukuza ufaulu lengo likiwa ni kuzipaisha kwa ajili ya kuvutia soko.
Kama mdau wa elimu, Bwire anasema tuhuma za rushwa ni uvumi tu lakini ukweli ni kuwa shule nyingi za binafsi zilizo makini zinafanya vizuri kutokana na kuwekeza katika mikakati na juhudi.
“Kwa mfano, tuchukulie shule yetu ya Alliance kwa taratibu zetu tulizojiandalia, mwanafunzi akifika darasa la sita lazima akae bweni, lazima saa 11:00 jioni ahudhurie vipindi na akae mpaka saa 3:30 usiku kila siku,” anasema.

Post a Comment

أحدث أقدم