CAG: Wabadhirifu, mafisadi sasa kukiona

Bagamoyo. Naibu Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Jasper Nicholaus Mero amesema pamoja na pongezi ambazo Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi inapokea, wananchi wa kawaida wameonyesha kutoridhishwa na hatua zinazochukuliwa dhidi ya watu wanaobainika kufuja mali za umma, kutumia mamlaka yao vibaya kwa mujibu wa ripoti za CAG.
Akizungumza jana katika ufunguzi wa kongamano la matumizi ya ripoti za ukaguzi kwa vyombo vya uchunguzi na wataalamu mbalimbali, Mero alisema kongamano hilo linalofanyika kwa mara ya kwanza ni sehemu ya utekelezaji wa shughuli za mradi wa kuongeza mapambano dhidi ya rushwa chini ya ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Uingereza (DFID).
Alisema kongamano hilo la siku mbili linalowahusisha maofisa wa DCI/PCCB 40, mahakimu 20, mawakili wa serikali 20 pamoja na wengine linalenga kutoa elimu kwa maofisa hao ili kupambana na walaghai, walarushwa na mafisadi.
“Tukiwa wadau katika maendeleo ya nchi yetu, tunao wajibu mkubwa wa kusimamia uwajibikaji na utawala bora. Ni vyema sasa tukatumia fursa hii ya mahusiano ya kisheria kuboresha utendaji kazi wetu ili kurejesha imani ya wananchi tunaowatumikia,” alisema Mero.
Aidha, alisema mpango huo utaongeza ufanisi zaidi katika utekelezaji wa matakwa ya sheria ya ukaguzi.
“Kifungu cha 27 cha sheria ya ukaguzi wa umma ya mwaka 2008 kama kilivyofanyiwa mabadiliko na Sheria ya Fedha no. 10 ya mwaka 2010, kinawataka wakaguzi wanaofanya kazi kwa niaba ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, mara tu anapobaini kuwapo kwa viashiria vya ulaghai, kughushi au rushwa wanapokuwa wanafanya ukaguzi kutoa taarifa kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu juu ya suala hilo,” alisema.

Post a Comment

Previous Post Next Post