
Nzega. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema), Freeman Mbowe amewatuhumu vigogo wa Serikali kwa ufisadi wa
Dola 600 milioni za Marekani, sawa na Sh1.2 trilioni walizotumia katika
mradi wa ujenzi wa Bomba la Gesi kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam.
Bomba hilo lililoanza kujengwa mwaka jana,
litasafirisha gesi asilia kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam ili
kuongeza vyanzo vya nishati ya umeme nchini.
Akihutubia wafuasi wa chama hicho jana kwenye
ziara yake ya ‘Operesheni Delete CCM’ (ODC), Mbowe alidai kuwa fedha
hizo walizojiongezea vigogo hao zimesababisha mradi huo sasa kugharimu
Sh2.40 trilioni.
Alisema kuwa awali kampuni inayojenga bomba hilo,
ilisema gharama halisi za mradi huo ilikuwa Sh1.20 trilioni, lakini wao
wakaongeza mara mbili ya fedha hizo kwa manufaa yao binafsi.
Mbowe aliwaeleza wafuasi hao kuwa, vigogo wa ngazi za juu serikalini wamegawana kiasi hicho cha fedha kilichozidi.
“Huu ni ufisadi wa hali ya juu na nitathibitisha
maelezo yangu popote nitakapotakiwa kufanya hivyo. Inaniuma sana, fedha
hizi zitalipwa na Watanzania maskini, wakati nusu yake zimeingia kwenye
mifuko ya vigogo,” alisema Mbowe.
Alisema kwamba kwa sasa vigogo wa CCM wanatafuta
fedha za kugharimia uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 na kuwa ufisadi huo
utasaidia kufanikisha malengo yao.
“Nawaomba wafuasi wa vyama vyote vya siasa
tusibaguane kwa itikadi zetu za vyama, bali tushirikiane kupambana na
ufisadi huu unaozidi kuwaletea umaskini wananchi,” alisema Mbowe ambaye
anatembelea mikoa ya Tabora, Katavi, Kigoma, Morogoro na Dodoma.
Katika hatua nyingine, Mbowe alidai kuwa nusu ya
wabunge wa CCM wamekaa bungeni huku wengine wakisinzia, lakini wananchi
wanaowaongoza wana matatizo mengi yanayohitajika kutatuliwa kwa pamoja.
Mbowe alieleza kuwa yeye ameacha posho ya
Sh300,000 na kufanya ziara kwa kutumia fedha zake binafsi kwa lengo la
kuwaelimisha wananchi.
“Pale bungeni hamna jambo la maana linalofanyika
zaidi ya kwenda kufuata posho. Ndiyo maana nimeamua kuondoka na kuachana
na posho zao, ili nije niwape elimu,” alisema Mbowe.
Katika operesheni hiyo, Mbowe aliendelea
kuvisisitizia vyama vya upinzani kushirikiana katika mambo wanayoyaamini
kuwa ni ya msingi kama vile kuing’oa CCM.
- Mwananchi
- Mwananchi
Post a Comment