Dk Chami: Viongozi wengi siyo wasafi

Moshi. Mbunge wa Moshi Vijijini, Dk Cyril Chami amesema kama Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma ingefanya kazi yake barabara, nusu ya viongozi wa umma wangepatikana na makosa.
Dk Chami amesema kama Tume hiyo inataka ifanikiwe, ianze na kazi ya kuwafunda Watanzania na watumishi wa umma waache kupenda njia ya mkato katika kupata mafanikio ndipo ihakiki mali zao.
Mbunge huyo ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara 2010- 2012, alitoa kauli hiyo hivi karibuni katika mahojiano maalumu na gazeti hili kuhusiana na masuala mbalimbali ya mustakabali wa nchi.
“Tume kama ilivyo haiwezi kufanikiwa kama Watanzania tutaendekeza ubinafsi na kupenda njia za mkato. Itamwadabisha nani kama mfumo wote una matatizo? Itawafunga wangapi?” alihoji Dk Chami.
Tume hiyo ipo chini ya Mwenyekiti wake, Jaji mstaafu Hamis Msumi na kumekuwa na hisia kutoka kwa wananchi kuwa haina meno kutokana na viongozi wengi wa umma kujilimbikizia mali.
Dk Chami aliongeza kusema, “Kama Tume ingefanya kazi yake barabara nina hakika nusu ya viongozi wangepatikana na kosa moja au lingine. Hawa ni wengi mno.”
“Tatizo ni kwamba sisi Watanzania tumetokea kupendelea njia za mkato kuliko kupata kwa halali na kwa kufanya kazi kwa bidii na maarifa,” alisisitiza Dk Chami katika mahojiano hayo.
“Watanzania tunaamini kuwa ‘kamati ya ufundi’ itatupatia Kombe la Afrika na hata la Dunia badala ya mazoezi. Tunaamini kuwa uchawi utatufanya matajiri na siyo kuchapa kazi,” alisema.
Alisema hata leo ukimfungulia kijana mdogo duka na ukamkabidhi aliendeshe, usipomwangalia atakuibia. Watanzania wengi wanaamini katika ‘dili’ badala ya kuchapa kazi kwa bidii.
Kwa mujibu wa Dk Chami, kwa hali ilivyo hapa nchini, hata watu waadilifu hawatakiwi miongoni mwa jamii kwa sababu tu wanaonekana wanazuia ulaji wa watu wengine wenye ulafi.
“Na inatokea hata hao waadilifu wachache wanapopigwa vita na mahasimu wao, mamlaka zinawatosa waadilifu na kuwaacha wapenda mkato wanapeta,” alisema Dk Chami na kuongeza kusema:
“Jambo hili lisipodhibitiwa litaendelea kuididimiza nchi yetu kwa sababu na hawa waadilifu wachache wakichoka wakaamua nao kuwa na tamaa, nchi itakwisha kabisa”.

Post a Comment

Previous Post Next Post