
Moshi. Mbunge wa Moshi Vijijini, Dk Cyril Chami amesema kama
Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma ingefanya kazi yake barabara, nusu
ya viongozi wa umma wangepatikana na makosa.
Dk Chami amesema kama Tume hiyo inataka ifanikiwe,
ianze na kazi ya kuwafunda Watanzania na watumishi wa umma waache
kupenda njia ya mkato katika kupata mafanikio ndipo ihakiki mali zao.
Mbunge huyo ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Viwanda
na Biashara 2010- 2012, alitoa kauli hiyo hivi karibuni katika mahojiano
maalumu na gazeti hili kuhusiana na masuala mbalimbali ya mustakabali
wa nchi.
“Tume kama ilivyo haiwezi kufanikiwa kama
Watanzania tutaendekeza ubinafsi na kupenda njia za mkato. Itamwadabisha
nani kama mfumo wote una matatizo? Itawafunga wangapi?” alihoji Dk
Chami.
Tume hiyo ipo chini ya Mwenyekiti wake, Jaji
mstaafu Hamis Msumi na kumekuwa na hisia kutoka kwa wananchi kuwa haina
meno kutokana na viongozi wengi wa umma kujilimbikizia mali.
Dk Chami aliongeza kusema, “Kama Tume ingefanya
kazi yake barabara nina hakika nusu ya viongozi wangepatikana na kosa
moja au lingine. Hawa ni wengi mno.”
“Tatizo ni kwamba sisi Watanzania tumetokea
kupendelea njia za mkato kuliko kupata kwa halali na kwa kufanya kazi
kwa bidii na maarifa,” alisisitiza Dk Chami katika mahojiano hayo.
“Watanzania tunaamini kuwa ‘kamati ya ufundi’
itatupatia Kombe la Afrika na hata la Dunia badala ya mazoezi. Tunaamini
kuwa uchawi utatufanya matajiri na siyo kuchapa kazi,” alisema.
Alisema hata leo ukimfungulia kijana mdogo duka na
ukamkabidhi aliendeshe, usipomwangalia atakuibia. Watanzania wengi
wanaamini katika ‘dili’ badala ya kuchapa kazi kwa bidii.
Kwa mujibu wa Dk Chami, kwa hali ilivyo hapa
nchini, hata watu waadilifu hawatakiwi miongoni mwa jamii kwa sababu tu
wanaonekana wanazuia ulaji wa watu wengine wenye ulafi.
“Na inatokea hata hao waadilifu wachache
wanapopigwa vita na mahasimu wao, mamlaka zinawatosa waadilifu na
kuwaacha wapenda mkato wanapeta,” alisema Dk Chami na kuongeza kusema:
“Jambo hili lisipodhibitiwa litaendelea
kuididimiza nchi yetu kwa sababu na hawa waadilifu wachache wakichoka
wakaamua nao kuwa na tamaa, nchi itakwisha kabisa”.
إرسال تعليق