
WANACHAMA wa Chama Cha Mapinduzi, (CCM), 54 akiwemo Mwenyekiti wa
kijiji cha Pemba wilayani Tarime Mkoa wa Mara, Augustino Wantora,
wamejiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo, (CHADEMA).
Wanachama hao wa CCM walipokelewa juzi na Makamu Mwenyekiti wa Baraza
la Wanawake CHADEMA, (BAWACHA), Hawa Mwaifunga, kwenye mkutano
uliofanyika uwanja wa Kutehuguma Kata ya Pemba.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Wantora alisema kuwa wameamua
kuhama CCM baada ya chama hicho tawala kukumbatia wala rushwa na
kuwanyanyasa wale wanaoipinga.
"Nikiwa CCM nilikataa rushwa nikajenga maadui wengi, yaani wale wote
nilioziba mianya yao ya rushwa wakaamua kunishugulikia kwa hila na
uongo, sasa mimi na wenzangu tumeamua kuja CHADEMA…
"Tumekuja huku kwa sababu tunajua ni chama kinachopigania haki za
wanyonge, tutafanya kazi na wale wanaopenda kula fedha za wananchi
tutaendelea kuwadhibiti," alisema mwenyekiti huyo.
Katibu wa BAWACHA Taifa, Grace Tendega, aliwataka wananchi hao
kuhakikisha wanateua viongozi wenye sifa kwa ajili ya kugombea nafasi
mbalimbali za uongozi kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa
kufanyika Desemba 14 mwaka huu.
Alisema kuwa wahakikishe wanajua vema mipaka ya vijiji na vitongoji
vyao kabla ya kujiandikisha au kujaza fomu za kugombea, ili kuepuka
kuzuiwa kugombea au kupiga kura.
Kwa upande wake Katibu wa CHADEMA mkoani Mara, Chacha Heche,
aliwataka wampe taarifa pindi watakaposumbuliwa na polisi na viongozi
wa serikali kwa kutundika bendera za CHADEMA kwenye nyumba zao.
"Mkikamatwa na polisi kwa kosa la kujiunga na CHADEMA au kupepea
bendera mnipe taarifa mara moja nikakutane na hao polisi, kwa sababu
CHADEMA ni chama cha siasa kilichosajiliwa kisheria," alisema Heche.
Naye Naibu Katibu BAWACHA Taifa, Kunti Yusuph, aliwataka wananchi hao
kuhakikisha wanahamasisha, wanajitokeza kupiga kura na kuzilinda.
Alisema kuwa mabadiliko wanayoyataka watayapata kijijini hapo endapo
watajitokeza kwa wingi kumpigia kura kiongozi anayefaa ambaye
anapatikana CHADEMA
إرسال تعليق