Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana
Posted on November 27, 2014
Posted on November 27, 2014
Cha Cha Mapinduzi (CCM), kimesema kila aliyehusika katika kashfa ya
uchotwaji wa Sh bilioni 321 katika akaunti ya Tegeta Escrow iliyokuwa
imefunguliwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), abebe msalaba wake bila kujali
cheo chake na kwamba muda wa kulindana umekwisha.
Hayo yalisemwa jana na Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana
na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye walipokuwa wakihutubia
mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Ilulu mkoani Lindi.
Waziri wa nchi Ofisi ya Rais asiyekuwa na wizara maalumu, Profesa
Mark Mwandosya, alisema ni vema watu wanaotajwa katika kashfa hiyo wakae
pembeni ili kutoitia doa
serikali na chama tawala.
Profesa Mwandosya alitoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza na
wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), ambao pia ni wanachama wa
CCM.
“Kwa sasa hivi vikao vya chama na serikali vinaendelea, ni lazima
ripoti iwasilishwe bungeni, mambo yawe hadharani ili mbivu na mbichi
zijulikane.
“Kwa maoni yangu, naamini kabisa kuwa ni vema wale wote wanaotajwa
kwenye hili suala la IPTL, wakakaa kando ili kuepuka kukipaka chama na
serikali matope,” alisema Profesa Mwandosya.
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba
amemtaka Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa
Sospeter Muhongo, na Katibu Mkuu wake, Eliachim Maswi pamoja na
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema wajiuzulu kutokana
na kutajwa katika kashfa hiyo.
Katika mkutano huo, Nape alisema watakaobanika kuhusika katika kashfa hiyo, wanapaswa kuwajibishwa bila kujali nafasi zao.
“Katika hili naomba niseme kila ambaye atabainika kuhusika
achukuliwe hatua, kila mtu abebe msalaba wake mwenyewe. Hatutakubali
kuona watu waliohusika katika sakata hilo wanaachwa, lazima wachukuliwe
hatua.
“CCM tunaheshimu miiko ya uongozi na maadili, hivyo hili la Escrow lazima waliohusika wachukuliwe hatua,”alisisitiza Nape.
Kwa upande wake Kinana alisema muda wa viongozi ndani ya chama hicho kulindana umekwisha na uvumilivu sasa basi.
Kinana ambaye hakuzungumzia kabisa sakata la Escrow, alitumia nafasi
hiyo kuwaambia wananchi. “Si sawa mwizi kumlinda mwizi, haiwezekani
mtu anaharibu halafu anaachwa.
“Muda wa kulindana haupo tena ndani ya CCM. Uvumilivu umefika
mwisho. Muda wa kubebana na kuvumuliana sasa umekwisha,”alisisitiza
Kinana.
Alisema CCM haiko tayari kuendelea kulindana na kubebana wakati
mambo yanaharibika huku akisisitiza kazi ya chama hicho ni kuisimamia
Serikali.
CUF
Nacho Chama cha Wananchi (CUF), kimemtaka Waziri Mkuu Mizengo Pinda,
Waziri wa Nishati na madini, Profesa Sospeter Muhongo na wengine
wanaotajwa katika kashfa hiyo kujiuzulu wenyewe vinginevyo rais atengue
uteuzi wao.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana,
Mwenyekiti wa Chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba alisema viongozi
wengine wanaopaswa kuwajibika ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali(AG),Jaji
Frederick Werema na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliachim
Maswi.
Alisema licha ya hatua hiyo, pia akaunti zote za benki zinazotajwa
kupitisha fedha za Escrow ni vyema zikafungwa na fedha zirudishwe
serikalini.
Profesa Lipumba pia alitaka mmiliki wa Kampuni ya VIP Engineering,
James Lugemalila iliyokuwa na asilimia 30 za hisa IPT na mmiliki wa
Kampuni ya Pan Africa Power Solutions Ltd (PAP), Harbinder Singh Sethi,
aliyenunua kampuni hiyo ya kufua umeme, wafikishwe mahakamani.
Alisema chama hicho kimefikia uamuzi huo baada ya kuona ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG).
“Tanesco walipaswa kurejeshewa sh bilioni 321 zilizolipwa kwa ITPL
kati ya mwaka 2002 na 2012, kwa hiyo fedha zote za akaunti ya escrow
jumla ya Sh bilioni 306 ni mali ya tanesco na bado wanaidai IPTL bilioni
15.
“Kutokana na hali hiyo, watuhumiwa hao wanapaswa kufikishwa
mahakamani kutokana na kufanya ufisadi mkubwa wa namna hiyo wakati
wananchi wanaishi katika mazingira magumu,”alisema Profesa Lipumba.
Alisema katika ripoti hiyo pia imeonyesha kuwa kampuni ya PAP
haikununua kihalali asilimia 70 ya hisa za kampuni ya Merchmar ya nchini
Malaysia katika IPTL kwa sababu zilikua zimezuiwa na mahakama.
“PAP hawana hati halisi za hisa hizo, pia ilifanya udanganyifu katika
malipo ya kodi kwa kutoa nyaraka za uongo kuwa walinunua hisa kwa sh
milioni 6 badala ya dola milioni 20, hali iliyoikosesha serikali mapato
ya Sh bilioni 8.7.
“Kosa hilo pia linawahusu Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kanda ya
Ilala ambao walihusika katika kupokea kodi ya mauzo hayo,”alisema.
Prof. Muhongo
Katika hatua nyingine, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amesema hajiuzulu ng’o.
Akizungumza na MTANZANIA jijini Dar es Salaam juzi, Profesa Muhongo
alisema uamuzi wa kujiuzulu unaweza kusababisha rasilimali za wananchi
kuibwa zaidi.
“Siwezi kujiuzulu kwa ajili ya kauli za watu…nafanya kazi kwa maslahi
ya wananchi, kama kuna watu wanadhani nitajiuzulu ili nitengeneze
mianya ya kula rushwa, wamejidanganya… sijiuzulu ng’o,”alisema.
Alisema hafanyi kazi kwa ajili ya kusikiliza maneno ya watu, bali
kutetea rasilimali za wananchi, hivyo hawezi kuhusishwa na mambo
yasiyomuhusu.
“Hata ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG)
inaonyesha wazi sijala hata shilingi kumi, na siwezi kufanya hivyo kwa
sababu nawatumikia wananchi kwa nia na moyo mmoja. Wanaotaka ning’oke
wana mambo yao binafsi, narudia tena kusema sing’oki.
“Sijatenda kosa baya lolote, wezi, walarushwa na wababaishaji wananiogopa na kunihofia,” alisema.
Alisema mara nyingi vyombo vya habari vimekuwa vikimtuhumu bila ya kuwa na ushahidi.
“Sitaki kutetewa, bali wanapaswa kuandika habari zenye ukweli ambazo zimefanyiwa utafiti kabla ya kutoa hukumu,” alisema.
Pinda ausia serikali
Naye Waziri Mkuu Mizengo Pinda, amesema ili kuweza kuridhisha nyoyo
za Watanzania katika kashfa ya IPTL, ni lazima Serikali ijipange ili
kuweza kutoa majibu yatakayoridhisha kuhusiana na suala la IPTL.
Amesema kwa kipindi cha sasa Taifa linapita katika wakati mbaya na mgumu wa lala salama kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Kauli hiyo aliitoa jana mjini Dodoma alipokuwa akitoa hotuba ya
kumweka wakfu Askofu Mkuu wa Dayosisi ya Kati wa Kanisa la Anglikana
Tanzania, Dk. Dickson Chilongani, ambapo alisema hivi sasa kumekuwa na
kampeni za kuchafuana mbele ya jamii.
“Baba Askofu kipindi hiki ni kibaya tunasema lala salama, kubwa ni
Serikali kutoa maelezo yatakayotuaminisha kwa wananchi. Ila uadilifu
mkubwa unahitajika serikalini kwa sababu kuna mapesa.
“…Kipindi hiki ni cha lala salama kwa hiyo watu wengine wamekuwa
wakichafua wengine kwa ajili ya kutaka kupata madaraka ya nchi,” alisema
Pinda.
Chanzo: Mtanzania
إرسال تعليق