Elimu duni yakwaza kilimo cha ufuta Tandahimba

Tandahimba. Baada ya kupata mafanikio ya wastani katika kilimo cha ufuta, wakulima wa zao hilo, ambao wengi ni wale wanaohama makazi yao kwa muda kutoka Wilaya ya Tandahimba, Mtwara kwenda Lindi kwa ajili ya zao hilo, sasa wanalilia elimu ili waweze kupata mafanikio makubwa zaidi.
Baadhi yao wanasema licha ya kwamba wanafanya kazi hiyo kwa bidii kutokana na faida na matokeo mazuri ya haraka wanayoyapata, hakuna mtaalamu yeyote wa kilimo ambaye aliwahi kuwaelekeza kuhusu namna bora ya kilimo hicho.
Kati ya Novemba na Mei mamia ya wakulima katika Wilaya ya Tandahimba huyaacha makazi yao na kwenda kuishi mkoani Lindi katika wilaya za Liwale na Kilwa kwa ajili ya kusaka ardhi yenye rutuba inayofaa kwa kilimo cha ufuta.
Mbali na ardhi yenye rutuba, wananchi wa Tandahimba wanasema eneo kubwa linalofaa kwa kilimo katika wilaya yao limefunikwa na zao la kudumu la mikorosho, hivyo ardhi iliyobaki haitoshelezi kumudu mahitaji ya kilimo cha mazao mengine, ufuta likiwa mojawapo.
“Hakuna mtaalamu yeyote wa kilimo aliyetueleza kilimo bora cha ufuta, tunachotumia ni uzoefu kwa kuwa tunafahamu ufuta ni zao linalohitaji rutuba nyingi basi tunakimbilia maeneo yenye rutuba hiyo,” anasema Mohamed Kawanga ambaye ni mkulima wa Kijiji cha Mkwiti, Tandahimba na kuongeza:
“Ukilima hapa Tandahimba utalazimika kutumia mbolea nyingi kwa zao la ufuta ambayo ni gharama kubwa, wakati mtu ukienda Lindi kuna eneo kubwa lenye ardhi nzuri, hivyo ni rahisi kulima na hakuna gharama za ziada.”
Wilaya ya Tandahimba ina wakazi 227,514 kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya 2012, wanaoishi katika kilomita za mraba 2048.56, ambazo kati yake asilimia 90 zinafaa kwa kilimo.
Hata hivyo, asilimia 91 ya eneo linalofaa kwa kilimo limefunikwa na miti ya mikorosho ambayo ndiyo uti wa mgongo wa uchumi wa wakazi wake. Wilaya hiyo inaoonga za uzalishaji wa korosho ambapo msimu 2013/14 ilizalisha tani 32,000.
Siyo lazima kuhama
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa kama wakulima wa Tandahimba wangekuwa na elimu kuhusu kilimo cha zao hilo, pengine wasingelazimika kusafiri hadi nje ya mkoa wao kwa ajili ya kilimo cha ufuta, kwani elimu hiyo ingewawezesha kulima zao hilo katika wilaya yao, hoja ambayo inaungwa mkono na wataalamu wa kilimo mkoani Mtwara.
Mkazi wa Nannala, Rashidi Mkadimba anasema kilimo cha ufuta kinaendeshwa kwa mazoea kutokana na wakulima kutokuwa na elimu ya kilimo hicho.
“Sisi kwetu hapa Nannala hatujui chochote cha kitaalamu kuhusu kilimo cha ufuta, hata huko Lindi tunapokwenda tunalima tu bila kufuata kanuni za kilimo kutokana na kutozifahamu,” anasema Mkadimba.

Post a Comment

أحدث أقدم